Rais Joyce Banda awali alitaka matokeo ya uchaguzi huo kufutiliwa mbali
Uchaguzi mkuu wa Malawi umeendelea kubeba sura mpya
ya sarakasi za mapingamizi ya kisheria, baada ya mahakama kuu ya
Lilongwe kuamuru Tume ya uchaguzi nchini humo iendelee na mipango ya
kazi zake bila kuingiliwa na mamlaka yeyote.
Uamuzi huo umetokana na ombi la chama cha Malawi
Congress MCP kutaka mahakama hiyo izuwie amri ya Mahakama kuu ya
Blantyre iliyo iamuru tume ya uchaguzi kuhesabu kura na kumtangaza
mshindi ndani ya siku 8, likiwa ni ombi la chama cha DPP.
Mwandishi wa BBC Baruan Muhuza aliye
mjini Lilongwe anasema kuwa uamuzi huo sasa una maana kwamba MCP
imeshinda kesi ambapo pamoja na mambo mengine wanataka kazi ya kuhesabu
kura ianze upya nchi nzima jambo ambalo ndiyo maamuzi ya tume na vyama
vyote vya siasa isipokuwa DPP.
Tume ya uchaguzi inakutana mjini Blantyre na itatoa taarifa baadaye kuhusu uamuzi uliochukuliwa na Mahakama Kuu hii leo.
Huku ikijulikana wazi kuwa kinachosubiriwa sasa
ni ama kurudiwa kuhesabu kura za maeneo yenye mgogoro au kura zote za
nchi nzima.
'DPP waja juu'
Jumamosi mchana tume ya
uchaguzi kwa pamoja na vyama vya siasa walikubaliana kurudia kuhesabu
kura zote kutokana na kugundulika makosa mengi katika baadhi ya maeneo,
huku DPP ikigomea hatua hiyo na kuamua kwenda mahakama kuu mjini
Blantyre kuzuia mpango huo ikitaka zihesabiwe zile tu zinazotiliwa
mashaka.
Jaji Lloyd Muhara wa mahakama hiyo alikubaliana
na ombi la DPP jambo ambalo pia likazua upya mgogoro wa kisheria ambapo
vyama vingine vikaungana kwa pamoja na wagombea binafsi kupeleka zuio
kwenye mahakama kuu ya Lilongwe chini ya kundi la wanasheria zaidi ya 12
wa chama cha MCP.
'Wizi wa kura'
Vijana kwa wakongwe wote walijitokeza kushiriki uchaguzi huo ambao wadadis wanasema umegeuka sarakasi
Uchaguzi wa Malawi umekumbwa na wimbi la
mivutano miongoni mwa vyama vikuu vya siasa vilivyo simamisha wagombea
urais wa nchi hiyo.
Dalili za kujitokeza kwa matatizo zilianza
mapema siku mbili baada ya uchaguzi ambapo baadhi ya vyama kikiwemo
chama tawala Peoples Party cha Rais Dr Joyce Banda walilalamika kuwa
kuna mchezo mchafu umefanyika katika shughuli nzima ya upigaji kura.
Siku chache zilizopita Rais Banda alitoa amari
ya kuufuta uchaguzi huo na kuitisha uchaguzi mwingine baada ya siku 90
kwa madai ya wizi na ulaghai uliokumba uchaguzi, lakini Mahakama kuu
ilisema hana mamlaka hayo.
Siku mbili baadaye tume ya uchaguzi MEC chini ya
mwenyekiti wake Jaji Mackson Mbendera, ikatangaza kuwa ni kweli
imegundua ubadhirifu katika baadhi ya maeneo na hivyo lazima kura zote
zihesabiwe upya.
Kufikia sasa haijajulikana nini itakuwa hatma ya
kura zilizopigwa na wananchi zaidi milioni saba wa nchi hiyo huku vyama
vya DPP na MCP kila kimoja kikidai kuwa kilielekea kushinda uchaguzi
huo