Thursday, May 29, 2014

LAPF YAMKANA KUMDAI MBOWE PIA YAWAKANA KUWASAIDIA MSIGWA NA MBILINYI


Mbowe, Hawa ghasia na Peter Msigwa
SIKU chache baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali za Mitaa Tawala za Mikoa (Tamisemi), Hawa Ghasia, kusema kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amekopa kiasi cha sh bilioni moja kwenye Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Eliud Sanga, amekanusha.

LAPF pia imekana kuwasaidia fedha au vifaa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi na Iringa Mjini, Peter Msigwa, kama ilivyosemwa bungeni. Juzi, Ghasia alisema kuwa Mbowe anadaiwa sh bilioni moja na LAPF na ametumiwa waraka wa kumkamata ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria. Waziri huyo alisema si kosa kwa wabunge kupewa fedha na LAPF, lakini ni kosa kwa mbunge kutorejesha fedha alizokopeshwa.

Kauli ya LAPF
Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Sanga, alibainisha kuwa LAPF haijawahi kumkopesha Mbowe sh bilioni moja, na kwamba mfuko huo hauna utaratibu wa kukopesha mtu mmoja mmoja, hivyo hakuna mikopo ya aina hiyo.
“Mfuko wa LAPF hauna utaratibu wa kukopesha mtu mmoja, hivyo hakuna mikopo ya aina hiyo na wanachofanya ni kutoa mikopo ya wanachama wake kupitia vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) na mikopo ya nyumba kwa wanachama wanaokaribia kustaafu,” alieleza Sanga.
Alisema shughuli kuu za mfuko huo ni kuandikisha wanachama, kukusanya michango, uwekezaji na kulipa mafao. “Ieleweke kuwa ingawa waheshimiwa wabunge au mtu au taasisi yoyote hazuiliwi kuomba msaada wa kijamii, Mbilinyi na Msigwa hawajawahi kuwasilisha maombi na hawajawahi kupewa msaada wowote na LAPF.

No comments:

Post a Comment