SIASA




Mambo 6 yanayomfanya mtu awe kiongozi bora na sio bora kiongozi
Tukiacha mbali picha ambayo mara nyingi au kwa miaka mingi imekuwa ikijengwa vichwani mwa wengi wanapoona na kudhani kwamba fulani ni kiongozi bora [pengine kwa muonekano tu], au kwa sababu anashuka kutoka kwenye gari kwa mbwembwe, tabasamu baada ya kufunguliwa mlango na mkanda na kisha kupokelewa briefcase yake, yapo mambo kadhaa ambayo yanamfanya mtu awe kiongozi bora na sio bora kiongozi. Na kadri siku zinavyokwenda, taswira ya kiongozi kwa muonekano tu inazidi kupotea. Vitendo,maadili,mafanikio, uvumbuzi na maendeleo vinachukua mstari wa mbele.

Tofauti na miaka ile ambayo picha ya kiongozi bora ilikuwa kama hiyo hapo juu, siku hizi viongozi bora wapo na wanajitokeza katika hali tofauti tofauti kabisa. Anaweza kuwa asiyevaa suti kama Dalai Lama na akawa kiongozi bora. Au asiyevaa suti bali t-shirt na jeans tu kama alivyokuwa Steve Jobs wa Apple au Mark Zuckerberg boss wa Facebook. Mifano ya viongozi hawa ipo mingi.
Kituo cha utafiti na mafunzo ya uongozi cha Dale Carnegie cha jijini New York nchini Marekani kinasema katika utafiti wao wamegundua kwamba kinachomfanya mtu awe kiongozi bora sio suti, briefcase, tabasamu[ hususani lile la uongo] bali uwezo na nia ya dhati katika kuamsha ari, kuwawezesha unaowaongoza, kuwafanya wajiamini na kuwapa motisha watu unaowaongoza.
Pamoja na hayo, na kutokana na ukweli kwamba leo hii tuna kila aina ya viongozi, yapo baadhi ya mambo yanayowatofautisha viongozi bora na bora viongozi. Haya hapa ni baadhi yake;
1. Aweze Kuyakabili Matatizo au Changamoto
Kiongozi bora ni yule ambaye ana ujasiri wa kutosha wa kukabiliana na kila aina ya changamoto au matatizo ambayo yanaweza kujitokeza iwe aliyatarajia au hakuyatarajia.
Dunia ya leo imejaa changamoto za kila aina. Kila kukicha kuna jipya na gumu zaidi. Uchumi umeporomoka, fedha haina thamani tena, kimbunga kikali kimekuja na kuipindua juu chini shule ya kijiji. Kiongozi bora anafanyaje? Anapotelea mjini kwa kisingizio cha kuwa “bize” au anakuwepo bega kwa bega kutatua tatizo?
Jibu lipo wazi. Kiongozi bora atakuwepo na kuwasiliana na kila mtu anayemuongoza iwe ni ofisini au jimboni kuhusu ukweli halisi na ukubwa wa tatizo na jinsi ambavyo yeye kama kiongozi analishughulikia [kwa kushirikiana na kila mtu wakiwemo anaowaongoza] tatizo au changamoto husika.
2.Awe Muaminifu
Kiongozi bora lazima awe muaminifu. Uaminifu unaanzia kwenye kuwa mkweli. Anaposema atafanya hili au lile, alifanye. Asipolifanya, awe muwazi na kuwaeleza wale anaowaongoza ukweli wa sababu zilizofanya asitimize ahadi yake na jitihada anazofanya kutimiza ahadi yake.
Kwa mfano wananchi wanapomchangua “kiongozi” kutokana na sera na ahadi za kutatua tatizo la ukosefu wa maji safi jimboni kwao kisha miaka mitano baadae ahadi hiyo ikawa haijatimia, ni wazi kwamba imani kwa kiongozi huyu itafifia kama sio kupotea kabisa. Mbaya zaidi pale atakapokuja na sababu ambazo hazina mashiko huku kila mtu akiona wazi kwamba ahadi yake ilikuwa ahadi hewa au ya kisiasa.
Onyesha kwamba unawajali na kuwathamini unaowaongoza. Yaelewe matatizo na changamoto za unaowaongoza. Shirikiana nao bega kwa bega kuyatatua. Usiwe kiongozi wa ofisini tu bali nenda kule walipo. Na usiende kwa nia ya kupigwa picha tu. Ili wakuamini ni muhimu wakaona kwamba wewe sio “mwizi” tu wa fursa.
3.Kuwa Halisi [Asiwe Feki]
Mojawapo ya mambo ambayo sio tu yanamfanya mtu awe bora kiongozi bali apoteze kabisa hata nafasi ya kuongoza ni pamoja na kuwa “feki”. Ni rahisi sana kwa mtu/watu kutambua kwamba huyu si yeye. Anajifanya kuwa mtu ambaye siye.
Kwa bahati mbaya hakuna mtu anayependa “feki”. Viongozi wanasiasa huanguka sana kwenye mtego huu. Wengi wanadhani wananchi hupenda kusikia mashairi na ngonjera tamu tamu pekee. La. Labda zamani. Siku hizi ukiwa kitimbakwila utajulikana kirahisi na utakuwa nje ya ulingo. Wenzetu wanasema Walk The Walk and Talk The Talk.
Hata kama wewe ni kiongozi wa ofisi au mfanyabiashara, pindi tu utakapokuwa “feki” wateja wako watajua. Watakukimbia. Watahisi hata vitu unavyouza ni “feki” kwa sababu wewe mwenyewe unaonekana feki au unajibeduisha kuwa sivyo. Kuwa orijino. Unapenda kucheka au kuchekesha? Cheka. Wachekeshe unaowaongoza. Unapenda muziki? Usihofu kuonyesha wazi kwamba unapenda muziki. Tumia vitu unavyovipenda au maarifa unayoyamudu zaidi kutengeneza aina yako ya uongozi.
4. Ajiheshimu
Kiongozi bora lazima ajiheshimu. Na dhana ya kujiheshimu ni pana. Kuna kujiheshimu katika nyumba na mahusiano yako iwe na wanao, mkeo, wazazi wako, ndugu, jamaa na hata marafiki. Kuna kuiheshimu ofisi yako na watu unaowaongoza. Kiongozi ambaye kila siku anakabiliwa na tuhuma za ulaji rushwa, uongo, umalaya ni wazi kwamba hajiheshimu na hivyo ni ngumu kuwafanya watu wengine wamheshimu. Nawajua baadhi ya “bora viongozi” ambao wametumbukia huko kutokana na tabia zao za ufuska ambazo ingawa wanahisi watu hawajui, kwa kiasi kikubwa zimewapotezea heshima ya uongozi na hususani uongozi bora.
Unapojiheshimu, inakuwa rahisi kuongoza wengine. Hakuna mtu anayependa kujishirikisha na mtu asiyejiheshimu. Watu hujisikia faraja kuhusiana au kufanya biashara na watu wanaojiheshimu. Pia hata kama unaongoza ofisi au biashara tu,wateja wenye akili timamu wanataka kutumia hela zao mahali ambapo ofisi au biashara inaheshimu na kutimiza ahadi zao kufuatana na misingi. Ukisema kwamba ninyi ndio duka lenye bei chee zaidi na bidhaa halisi, basi iwe ni kweli. Vinginevyo inaashiria kwamba hamjiheshimu. Ni waongo. Uongo ni sehemu ya kutojiheshimu.
5. Jifunze/ Taka Kujua Zaidi/ Nenda Na Wakati
Kiongozi bora ni yule ambaye anataka kujifunza zaidi na ni mtafiti. Mwisho wa darasa sio mwisho wa kujifunza kwa kiongozi bora. Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini aliwahi kunieleza katika mahojiano yangu naye jinsi ambavyo alishangaa wakati fulani kusafiri na viongozi fulani kutoka Tanzania mpaka Ujerumani na asione wakisoma hata vipeperushi vinavyokuwa kwenye viti achilia mbali vitabu,magazeti nk.Viongozi bora wanauliza maswali. Wanauliza maswali kwa nia ya kujifunza, kupata maarifa na taarifa. Ni wasikivu na wapo tayari kufundishwa.
Kwa bahati nzuri dunia ya leo ina kila nafasi na uwezekano wa kujifunza. Hizi ni zama za sayansi na tekinolojia. Kiongozi bora atataka kujua…hicho kitu kinachoitwa Twitter ni nini? Kinafanyaje kazi? Atajiunga. Atataka kujua jinsi watu wanavyowasiliana siku hizi. Atataka kujua jinsi nchi za wenzetu wanavyofanikiwa katika masuala mbalimbali. Atajitahidi na kuchunguza mpaka mwisho kuona kama sayansi hiyo au maarifa hayo yanaweza pia kutumika nchini kwake,jimboni kwake, ofisini kwake nk. Kiongozi bora atasoma vitabu,majarida,magazeti, nk kwa nia ya kujifunza zaidi.
6. Kuwa Mtendaji
Yote niliyoyataja hapo juu yanakamilishwa au kuhusishwa moja kwa moja na utendaji. Kiongozi bora haishii kwenye kuongea tu huku akijizungusha kwenye kiti na kuagiza chai. La.Anatenda. Ananyanyuka, kwenda na kutenda kama mfano. Tunapomkumbuka Mwalimu Nyerere kama kiongozi bora aliyewahi kutokea ni kwa sababu alikuwa mtendaji.
Aliongea,kuelekeza,kuonya lakini mwisho wa siku alikuwa mtendaji.
Nyanyuka na enenda ukaifanye kazi. Onyesha kwa vitendo kwamba wewe ni kiongozi bora na sio bora kiongozi.
UMASIKINI WA MAWAZO NI UMASIKINI KUPITA UMASIKINI WOTE- BY J.K.NYERERE (R.I.P)

 31/10/2011






JELA NI MAHALI PA KUISHI KAMA SABABU YA KWENDA HUKO NI VITA DHIDI YA UONEVU, UKANDAMIZAJI WA HAKI NA UTU WA BINADAMU.
 Wapendwa wapiga kura wangu na Watanzania wenzangu. Sina wakati mgumu kuchukua maamuzi haya yanayotokea leo. Upendo huu nilio nao kwa watu wa Arusha na nchi yangu ni sababu ya msingi ya maamuzi haya. Nimetishwa mara nyingi, rafiki zangu wametishwa, jamii ya watu duni imeendelea kuishi kwa mashaka na matisho kwa muda mrefu.

Katika mazingira haya, nikawaza sana kuwa anatakiwa kutokea mtu mmoja jasiri atakayeweza kuona thamani ya watu wengine. Huyo mtu anaweza kuwa wewe lakini kwa wakati huu siwezi kumsubiri tena na nimechagua kuwa mimi nikiamini kuwa utanikuta nikiendelea na safari ya ukombozi.

Tupo wengi sana tunaotaka mabadiliko, haki na ukweli. Hata hivyo hofu, woga na mashaka yamepoteza thamani yetu yote ya maana ya kuishi.

Waliofungwa kwa kuonewa na kuteswa, waliokosa chakula na kulala nje, waliokwenda hospitali na kukosa madawa, waliokosa ajira na kipato mpaka kujikuta wametoroka familia zao, waliopoteza matumaini ya maisha, waliopora utajiri wa nchi yetu kwa manufaa yao binafsi, walionunua haki na sheria dhidi ya wajane na wanyonge na kuwapora vipato vyao vidogo na mashamba yao, USIULIZE SABABU NINI!

Nimetafakari sana na nikatambua kuwa sababu ni mimi pale nilipokuwa kimya wakati wajane na wanyonge wanaonewa.

NIliposikia wengine wanaandamana kupinga uovu, uonevu, wizi, ufisadi na ukandamizaji wa haki nikasema ni hao na wala sio mimi, kumbe nilipaswa kuwa mbele katika harakati hizi.

Nilipoona wenzangu hawawezi kupata matibabu nikasema mimi sio mgonjwa, nilipopata taarifa za rafiki zangu kufungwa kwa makosa yasiyo yao, nilipoona watoto wa mitaani wanaomba chakula, nilipoona wazee
wamepoteza matumaini ya kuishi katika uzee wao, nilipoona vijana hawana ajira, nilipoona mabinti wasichana wadogo wameamua kufanya biashara ya ukahaba, NIKATAFAKARI,TENA NIKATAFAKARI, dhahabu zetu, almasi yetu, Milima na mabonde yetu, Tanzaninte yetu, samaki wetu, Uranium yetu, makaa ya mawe yetu, utalii wetu, ardhi na kilimo chetu na zaidi utu na mahusiano yetu.

Na sasa siwezi kukaa kimya tena. NI afadhali vita inayotafuta haki na usawa kuliko amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa mwanadamu. Na katika msingi huu hofu na mashaka vimekosa thamani kwangu, sitamwogopa mtu yoyote, mwenye silaha yoyote, mwenye cheo chochote na wala sitaogopa jela yoyote katika kupigania haki, utu wa kweli katika jamii yangu.

Wanafikiri wataendelea kutuogopesha kwa sababu wana jela na silaha, wanafikiri tutaendelea kuabudu uoga, wanafikiri wataendela kutunyanyasabila sababu ya msingi LAKINI SISI TUNAJUA TUTASHINDA KWA SABABU HAKI TUNAYOIPIGANIA NI MAKUSUDI YA MWENYEZI MUNGU.

Leo nitakwenda jela kwa hiari yangu binafsi kwa siku kadhaa na si kwa NIA YA KUJITAFUTIA UTUKUFU WANGU bali ,” JELA NI MAHALI PA KUISHI KAMA SABABU YA KWENDA HUKO NI VITA DHIDI YA UONEVU, UKANDAMIZAJI WA HAKI NA UTU WA BINADAMU.

Kila mara nilipotishiwa nikagundua wanaonitishia, wananitishia kwa jela na mauti. Na mimi nikagundua na nikatambua ni afadhali kuishi miaka hamsini jela huku sababu ikiwa ni kupinga uonevu na ukandamizaji kuliko maisha ya woga na anasa yasiyo na kusudi katika kutetea utu na heshima ya mwanadamu mwenzangu.

Wale mlionitishia kunipeleka jela sasa nimetangulia kwa hiari yangu na wale mliobaki msiogope jela endeleeni kupigania ukombozi utakaoleta usawa katika nchi yenu.

Watakaotubeza na kututukana wasameheni kwani wanahitaji ukombozi wa fikra, watakaotupongeza na kutuonea huruma wafundisheni ujasiri na waambieni mapambano bado yanaendelea tunahitaji umoja wao. Nitarudi mapema.

MSIOGOPE, MSIOGOPE, MSIOGOPE, MUNGU YUPO UPANDE WETU.

Hata kama sipo arusha, na si mwenyeji wa Arusha I wish we could have ten people like him, Tanzania yenye Neema Ingepatikana kwa vyovyote vile.........

Let him have long life and lets wait if he is going to behave contrary......




MALCOM X

Born May 19, 1925 in Omaha, Nebraska, this fiery black nationalist leader was a charismatic spokesman for the Nation of Islam until breaking with the group shortly before his 1965 assassination


GODBLESS LEMA

"Ni heri ya vita inayotafuta haki na usawa kuliko Amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa Mwanadamu"

No comments:

Post a Comment