@Mwanamabadiliko
KATIKA
hili bunge la bajeti linaloendelea sasa hivi, pamoja na kwamba limekosa
mvuto kutoka kwa jamii ya watanzania, kuna mambo matatu nimeyagundua.
Kwanza, huu utaratibu wa kuondoa shilingi kwenye mshahara wa waziri ni
kama mchezo wa kuigiza kwa kuwa wabunge wanaoshika hizo shilingi
hatimaye huziachia na vifungu vya ovyo vya bajeti hupitishwa.
Pili,
kwa mara ya kwanza katika historia ya bunge hili nimeshuhudia wabunge
wa CCM wakiondoa shilingi kwenye mshahara wa waziri wa chama chao.
Nadhani ni muendelezo ule ule wa kuleta mzaha na kuwakoga wananchi
wanaowatazama ili waone kwamba wana uchungu na maendeleo yao wakati si
kweli.
Lakini pia
wanafanya hivyo ili kufuata mkumbo wa wabunge wa UKAWA ambao tangu
mwanzo walitahadharisha kushika shilingi za mishahara ya mawaziri ambao
wameshindwa kuleta maisha bora kwa kila mtanzania. Kinachowaponza
wabunge wa UKAWA ni uchache wao kwani hata kama wakishika shilingi,
mwisho wa siku wabunge wa CCM watapiga kura za Ndiyooooooooooooooo ili
kuwaokoa mawaziri wao wa CCM.
Tatu,
nimegundua kwamba mle bungeni kuna wabunge wa CCM ambao wao kazi yao
kubwa wanayoijua ni kusema NDIYOOOOOOOOOOO kwa sauti kubwa ili vifungu
vya bajeti, hata vile vibovu, vipite bila kupingwa. Kundi hili huwa
halichangii chochote bungeni. Wakishaingia bungeni wakasaini kwenye
kitabu cha posho, hukaa mezani na kusubiri kugonga meza.
Hili ni suala la
kustaajabisha sana kwani wabunge hawa wametumwa na wananchi waende
kuwawakilisha lakini wamegeuka kuwa wachumia tumbo na watetezi wa
ukandamizaji wa serikali dhidi ya wananchi.
Na kwa kuwa moja ya
kazi ya wabunge ni kuibana serikali iwahudumie wananchi, wabunge hawa
wa CCM ni wasaliti wa wapiga kura wao na hawafai kurejeshwa bungeni tena
msimu ujao. Inasikitisha sana kuona kwamba wabunge hawa wa CCM wapo
bungeni kwa lengo la kuwakandamiza wananchi badala ya kuwatetea!
No comments:
Post a Comment