Friday, November 28, 2014

TANZANIA; NCHI YA WATU WALIOZIDISHA UPOLE! INASIKITISHA SANA!!!!

 


TANGU mwaka 1961 nchi hii ilipopata uhuru, wanasiasa ambao wamekuwa  wakiingia na kutoka madarakani kupitia utawala wa chama kimoja, wamewalea Watanzania kwa kuwaaminisha kwamba amani na utulivu ndiyo mwisho wa kila kitu!

Rais Jakaya Mrisho Kikwete
 
Wanasiasa waadilifu na wahuni  katika majukwaa ya kisiasa ya nchi hii, wote kwa pamoja wamekuwa wakitoa ‘dawa’ hiyo kwa Watanzania  ili kulinda usalama wa nafasi zao na maslahi yao.
Matokeo yake, katika hali halisi, wanasiasa waovu  wameitumia fursa hiyo kuwalaghai Watanzania kwa njia hiyo ili kuwaziba midomo na kuwafunga mikono  wasiweze kutetea haki zao na kunyoosha vidole dhidi ya makosa yanayofanywa na walio madarakani.
Kwa kifupi, amani waliyofundishwa si kuishi vyema na majirani zao, bali kuishi vyema na watu walio madarakani!
Kutokana na woga huo hadi leo – 2014 – asilimia kubwa zaidi ya Watanzania wamebakia kuwa watu wa kutukuza amani na utulivu tu!  Wamekuwa wengi ni watu ambao hawajui kudai haki zao au kujitokeza waziwazi kupinga maovu yanayofanywa na watu wenye madaraka nchini.
Matukio makubwa yaliyotikisa nchi kama vile wizi wa fedha za EPA, Operesheni Tokomeza, Kashfa ya Richmond, Kashfa ya Rada, Wizi wa Fedha za Escrow na mengine  ambayo yaliongeza umaskini na unyonge kwa Watanzania, yalifanywa chini ya dhana ya malezi ya amani na utulivu!
Vitisho vya amani na utulivu vimewafanya Watanzania kuwa ‘toothless bulldogs’.  Hayo ni maneno ya Kiingereza yenye maana ya ‘mbwa wasio na meno’. Maana yake wamekuwa sawa na mbwa wenye maumbo ya kutisha, lakini midomoni ni viboboyo ambao huishia kubweka tu.
Kwa miaka nenda-rudi, Watanzania wamekuwa ni watu wenye kuishia  kunung’unika tu lakini hawachukui kitendo chochote cha kuonesha hasira na hisia zao dhidi ya maovu au mambo wasiyoyapenda kutoka kwa watawala.
Huruma ya Watanzania kwa wanasiasa imeendelea siku zote za maisha yao. Ujanja wao kikomo chao ni wanasiasa. Pamoja na vitendo lukuki vifanywavyo na watu walio madarakani katika kujinufaisha wao na familia zao, Watanzania hawa wapole kila wamwonapo mwanasiasa mbele yao, meno yao yote midomoni hung’oka wakashindwa kuuma na wakati huohuo wakayasahau matatizo yao.
Walioko madarakani wanaufahamu fika upole na ‘wema’ wa Watanzania.  Watafanya lolote watakalo, kisiasa, kiuchumi na kijamii, wakifahamu kabisa hawatapatilizwa na wananchi wao – hususan mamilioni yao ambao wengi wao hawana elimu na uwezo wa kuyafahamu yanayofanyika mijini na kwenye ofisi za maamuzi ya kisiasa.
Huo ndiyo mtaji wa wanasiasa wasio waadilifu. Watapora mali ya umma, wataendesha vitisho dhidi ya Watanzania ‘wajanja’ kwa kuwateka na kwenda kuwatesa kwa vipigo na kuwatoboa macho,
watapindisha matakwa ya umma kwa ajili ya maslahi yao na kadhalika, wakijua wazi kwamba hakuna atakayeinua kidole kupinga. Wanajua kabisa Watanzania ni wapole, ni sawa na mabonge ya mbwa yasiyokuwa na meno. Ni watu waliokubali kugeuzwageuzwa kama chapati.
Chini ya amani na utulivu, mtu atachukua twiga, tembo na swala na kuwapakia katika ndege na kuwapeleka nchi za nje, atafanya biashara akiwa ikulu. Atafanya biashara ya pembe za ndovu bila woga, atakula fedha za halmashauri ya wilayani kwake, yote haya akijua mtaji wake mkuu ni ‘Upole wa Watanzania’!
Hao ndiyo Watanzania wapole wanaompenda kila mtu wakati wengine duniani wakila pilau, wao (Watanzania) wanakula ‘amani na utulivu’! Watanzania tuamke, tuwakatae wezi wa taifa hili kisha tujikite kulinda rasilimali zetu.

No comments:

Post a Comment