Monday, July 21, 2014

NAPE: WANAOTAKA URAIS 2015 RUKSA KUTANGAZA NIA, KUPIGA KAMPENI KOSA LA 'JINAI'


NA BASHIR NKOROMO
CCM imeweka wazi kwamba kwa mujibu wa taratibu zake, wanaotaka urais kupitia chama hicho wako huru kutangaza nia, na kusisitiza kwamba ugomvi wake mkubwa ni kwa wanaofanya kampeni kabla ya wakati.
Imesisitiza kwamba, kitawachulia hatua stahiki kwa mujibu wa katiba na taratibu za chama, bila kuwaonea huruma wala aibu, kutokana na namna yoyote ikiwemo uwezo wa fedha, nafasi zao za uongozi au umaarufu walionao wale wote watakaobainika kutangaza nia na kisha wakafanya kampeni kabla ya muda rasmi, kwa namna yoyote kutaka kuwania kuteuliwa na CCM kuwania Urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Hayo yamesemwa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, wakati akizungumza katika kipindi cha 'Baragumu' kwenye Kituo cha Televisheni cha Chanel ten, leo Julai 21, 2014, kilichokuwa na mada 'Urais na Makundi ndani ya Chama'.

"kwanza kabisa Chama chetu kina wanachama wengi, tena wenye sifa za uongozi katika nafasi mbalimbali, katika wingi huu wa wanachama kutakuwa na watu wengi wenye uwezo wanaotaka urais na nafasi nyinge za uongozi, kwa maana hiyo kelele za kutaka zitakuwa nyingi kwa maana na ushindani na ndiyo maana wenzetu huvizia wawili watatu wanaokosa na kuwafanya wagombea wao", alisema Nape.

Nape alisema, wingi na ubora huu wa wanachama kuwa na sifa za kuwania uongozi ikiwemo urais, bado haiwezi kuwa sababu ya kuacha kila mmoja kutafuta nafasi kwa kupitia utaratibu anaotaka yeye, kila anayedhani kuwa anafaa kuongoza kupitia CCM, lazima kuhakikisha anazingatia kanuni za uongozi na maadili na kanuni za uchaguzi ndani ya CCM.

Alisema kwa mujibu wa kanuni ya Uchaguzi za CCM mwanachama anaruhusiwa kutangaza nia, lakini ni marufuku kuita watu na kuwashawishi kwa maneno, fedha au takrima vyote vikiwa na sura ya kampeni.

Nape alisema, lengo la kanuni hizo za chama ni kuzuia makundi ya mapema ambayo husababisha mtafaruku na mgawanyiko mkubwa ndani ya Chama jambo ambalo alisema, chama kinalikemea kwa lengo la kulinda imani na nguvu ya chama.

Alisema, baadhi ya waliotangaza nia ya kuwania Urais na kupewa onyo kali kwa kipindi cha miezi sita, baada ya kubainika kufanya kampeni kwa namna moja au nyingine,wasipojirekebisha, kwa mujibu wa kanuni wataongezewa adhabu ya karipio kali adhabu ambayo ni ya miezi 18, ambapo utekelezwaji wake utamfanya mhusika kukosa sifa ya kuwania uongozi wa ngazi yoyote kupitia Chama.

Nape alitoa mwito kwa wanaotaka kuwania uongozi hasa urais kwa tiketi ya CCM, kujitahidi kuzingatia kanuni na taratibu zilizopo, ili wasije wakapoteza sifa ya kuwania nafasi wanazotaka.

"Tena, mimi nawaambia hawa, waache kujaribu kujenga makundi kabla ya wakati kwa sababu hata wao hawatanufaika, maana hata wakija wakapata kuteuliwa huku CCM ikiwa vipande vipande hawatapata wanachotaka", alionya Nape.

No comments:

Post a Comment