Mshambuliaji wa Lille ya
Ufaransa , Mkenya Divorc Origi ambaye ni mzaliwa wa Ubelgiji ni miongoni
mwa wachezaji wa timu ya taifa ambayo imeondoka Jumanne kuelekea Brazil
kwa mashindano ya kombe la dunia kuanzia Alhamisi wiki hii.
Origi, mwanae Mike Okoth, mchezaji wa zamani wa
timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars atakua mchezaji wa kwanza wa
Afrika Mashariki kuiwakilisha Ubelgiji, na yuko pamoja na wachezaji
nyota kama vile Vincent Kompany wa Manchester City na Eden Hazard wa
Chelsea.
Watakabiliana na Algeria mechi yao
ya kwanza ya kundi H Juni tarehe 17 na siku tano baadae wanapepetana na
Urusi kisha Korea Kusini kwenye mechi za mchujo.
Akizungumza na BBC kwa njia ya simu akiwa
Ubelgiji Origi anasema:'' Algeria ni timu yenye wachezaji wazuri kwa
hivyo hatuwezi kuidharau. Tutacheza mchezo wetu wa kawaida lakini nina
matumaini makubwa tutashinda.’’ Anasema Urusi na Korea pia si timu
hafifu hasa Warusi. Lengo lake kubwa ni Ubelgiji kufuzu kwa raundi ya
pili kisha kutoka hapo anasema mambo yatakuwa sawa kabisa.
Kuhusu mbona ameamua kuiwakilisha Ubelgiji na
sio taifa la babake Kenya, Origi anasema alitilia maanani mambo mengi
kama vile usimamizi mzuri wa kandanda nchini humo, mizizi yake ya
kandanda iliyoko huko, marafiki, ushauri wa babake pamoja na Ubelgiji
kufuzu kwa kombe la dunia kwani haijulikani ni mwaka upi Kenya itafuzu
kwa kombe la dunia.
No comments:
Post a Comment