Monday, March 31, 2014

DR. SLAA ;CHADEMA KWA SASA IMEUNGANA NA NCCR-MAGEUZI NA CUF NA KUUNDA UKAWA BUNGENI





BAADA ya kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ndani ya Bunge Maalum la Katiba, vyama vya siasa vya upinzani ,vimeunda umoja wa aina hiyo nje ya bunge hilo (UKAWA- nje) na kupanga kuwashawishi wananchi nchi nzima kudai Katiba yenye kujali maslahi yao.

Kwa mujibu wa makatibu wakuu wa vyama vinavyounda umoja huo ndani na nje ya Bunge hilo; CHADEMA,NCCR-Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF), lengo ni kuwahamasisha wananchi waunge mkono jitihada zinazofanywa na UKAWA kuhakikisha wajumbe wanafuata taratibu kuandaa Katiba mpya, ikiwa ni pamoja na kuzipa hoja za wananchi nafasi.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari Dar es Salaam jana, kwa niaba ya makatibu wakuu wenzake, Dk Willbrod Slaa kutoka Chadema alisema, utekelezaji wa malengo ya UKAWA-nje unaanza rasmi leo mkoani Mwanza, kwa kuzindua mkutano utakaohutubiwa na viongozi hao.

“Bada ya kufuatilia yanayoendelea katika Bunge Maalum la Katiba, sisi viongozi wa vyama vinavyounda UKAWA ndani ya Bunge, ambao tupo nje ya bunge hilo tumeona kuna umuhimu wa kuunda umoja huo nje pia kuhakikisha tunawaelewesha wananchi mambo yote wanayopaswa kuyaelewa kuhusu mchakato unaoendelea ili wakati wa kupiga kura ya kukubali au kukataa Katiba itakayopendekezwa wawe na uelewa wa mambo yote”.

“Tunajionea kinachoendelea bungeni sasa hivi na wala hatutaki kufanya jambo lolote litakalo ufanya mchakato wa kupata Katiba mpya uvurugike au kuvunjwa kabla ya muda wake kwa sababu kufanya hivyo hakutatusaidia wala kutuletea Katiba mpya tuliyoililia kwa miaka mingi...”

“Cha msingi kwetu ni kuwaunganisha wananchi na kuwaomba ushirikiano katika kuwahimiza wajumbe wafuate kanuni ili muda usiishe bila kutuletea Katiba tunayoitaka. Tunakwenda kuwaelimisha kwa mikutano ya hadhara, ili walilie Katiba inayojali maslahi ya watu na si ya chama chochote cha siasa au watu wachache.Tunataka wakisema ndio wafanye hivyo wakijua sababu na waseme hapana wakiwa na sababu,” Dk Slaa alisema.

Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Shaweju Mketo, alieleza kuwa nia yao kuu ni kutengeneza na si kuvuruga kama inavyofikiriwa na baadhi ya watu wanaovitazama vyama vya upinzani kama vurugu wakati hoja wanazoziibua ni kwa ajili ya kutengeneza.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema, hawategemei kuwaambia wananchi wagome wala kufanya vurugu katika mikutano yao kutokana na yanayoendelea bungeni, bali watawafundisha jinsi ya kudai Katiba mpya kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo.

Kwa hisani ya Habarileo.

No comments:

Post a Comment