Saturday, June 7, 2014

MAMBO USIYOYAJUA YALIYOFANYWA NA DR SLAA NA FREEMAN AIKAEL MBOWE NDANI YA CHADEMA

Nimekuwa mfuatiliaji wa wanasiasa mashuhuri Tanzania,Afrika na duniani kwa ujumla.Nimekuwa nikipenda kufanyia uchunguzi wanasiasa hawa walipoanzia harakati zao na mafanikio yao binafsi na ya wananchi wao wanaowaongoza.Nitakuwa nikijadili wanasiasa mbalimbali kwa awamu na leo ningependa nianze kuwajadili wanasiasa mashuhuri Tanzania, Freeman Mbowe na Dr Wilbroad Slaa.

Kwanini nimewachanganya Pamoja? Ni ukweli ulio dhahiri kwamba huwezi kuwatenganisha wanasiasa hawa wawili hasa unapojadili mafanikio ndani ya Chadema.Freeman Mbowe ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa na Wilbroad Slaa ni Katibu mkuu wa Chadema Taifa.Viongozi hawa wawili wamekuwa mhimili mkuu wa siasa za Chadema. Kitu kikubwa walicho nacho viongozi hawa wawili ni Ushirikiano wao.

Kila mmoja ana utaratibu wake katika uongozi lakini ushirikiano wao katika kazi umeifanya Chadema iwe moja na imara kama ilivyo.Ni vigumu kumsikia yeyote kati yao akisema kitu tofauti na mwenzake.Ninaamini hata kama kuna lolote ambalo wanakuwa hawakubaliani wanalimaliza ndani kwa ndani na kamwe humsikii yeyote akiongea tofauti na mwenzake.

Huu ndio uongozi unaotakiwa na hakika ndio siri kubwa iliyofanya Chadema ifike hapa ilipo.Kitu kikubwa kilichowapa credit kubwa viongozi hawa wawili ni pale Mwenyekiti Freeman Mbowe alipoachia nafasi ya kugombea urais kwa Katibu mkuu Dr Wilbroad Slaa.Kwa aina ya viongozi wa Afrika tulio nao ni vigumu sana kuona spirit ya aina hii.

Na endapo kama hili lingefanikiwa basi Tanzania kwa mara ya kwanza ingekuwa kama nchi za Ulaya na Marekani ambapo Rais wa nchi siyo mwenyekiti wa chama tawala.Lakini kingine kikubwa kinachowapa sifa wakuu hawa wawili ni wazi wanaongoza jopo la vijana mbalimbali wasomi na wenye nafasi mbalimbali za uongozi.

Tunajua kuongoza vijana ni kazi hasa tunaposema vijana bado damu inachemka,lakini vijana hawa wamefundwa na wanawatii viongozi wao mfano John Mnyika,Godbless Lema,Halima Mdee,Tundu Lissu,Ezekiah Wenje,John Heche,Joseph Mbilinyi-Sugu na wengine wengi.
Mafanikio yao Freeman Mbowe na Dr Wilbroad Slaa wamepata mafanikio makubwa katika uongozi wao ambayo hata tukiyataja hatuwezi kuyamaliza kwa leo.Lakini kwa uchache nitataja yale makuu.
1.Kuitoa Chadema kutoka Chama kidogo kabisa hadi kuwa Chama tishio na mbadala wa Chama Tawala
2.Kutoka wabunge 11 katika bunge lililopita hadi kufikia wabunge 48
3.Kuwa Chama kikuu Rasmi cha Upinzani nchini.
4.Kuwa Chama tulivu na kisicho na migogoro ya kipuuzi.
5.Kuwa msemaji na kimbilio la watanzania
6.Kuongoza operesheni mbalimbali nchini zilizoingiza maelfu ya wanachama na kufungua matawi kote nchini
7.Kukuza mapato ya Chadema kwa njia mbalimbali
8.Kujenga ngome yake kuu kwa wasomi hususani katika vyuo vikuu.
9.Kujenga demokrasia ndani ya chama
10.Kufuta kabisa ule usemi kwamba vyama vya upinzani ni vyama vya msimu.

Maadui wa Chadema wanatakaje? Katika uchunguzi wangu nimegundua kitu kimoja.Kwamba wale wote wasioitakia mema Chadema wanaamini njia pekee ya kukimaliza chama hicho ni kuwatenganisha viongozi hao wawili.Mtu mmoja alinipa mfano jinsi ilivyokuwa rahisi kuisambaratisha NCCR kutokana na tofauti za viongozi wake wakuu.Imekuwa ni rahisi zaidi kwa ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko kuivuruga Chadema chini ya Freeman Mbowe na Dr Wilbroad Slaa.
Ni ukweli kwamba Freeman Mbowe mwanasiasa na mfanyabiashara mwenye ukwasi mkubwa hapenyeki kirahisi.Kwanza maadui wengi wanapenda kutumia pesa kurubuni watu, sasa Freeman mtamnunua kwa bei gani? Hali kadhalika Dr Wilbroad Slaa msomi aliyebobea na kulingana na falsafa,hulka na itikadi yake amekuwa injini kuu ya chadema kwa nafasi yake ya Katibu mkuu ambapo ndiye mtendaji mkuu na msimamizi mkuu wa shughuli za siku kwa siku za chama.Sasa kwa hali hii na kwa vyovyote vile maadui wa chama hiki wasingependa umoja wa viongozi hawa wawili.
Changamoto zao. Penye mafanikio hapakosi changamoto.Kwa ufuatiliaji wangu niliofanya bado viongozi hawa wanatakiwa kuongeza juhudi zaidi katika kufungua matawi ya wanachama hadi kwenye mashina.Si vibaya wakatumia mfumo wa washindani wao wakuu CCM ambao wana utaraibu wa uongozi unaojulikana kama balozi wa nyumba kumi.

Njia hii imeisaidia sana CCM hasa nyakati za uchaguzi.Changamoto nyingine ni kuwa na ofisi kubwa na ya kisasa ya makao makuu inayoendana na hadhi ya chama hicho. Mwisho viongozi hawa wanatakiwa waandae program ya kuwapata wanachama wenye sifa na wanaofaa kugombea nafasi za serikali za mitaa,udiwani na ubunge.Chadema waachane na mfumo wa zima moto wa kupata wagombea.
Mwisho 
Kama nilivyoeleza juu viongozi hawa wawili Freeman Mbowe na Dr Wilbroad Slaa wamekuwa ni nguzo kuu ya chama hiki.Hapa Chadema kilipofikia kipo kwenye hatua ya mwisho yenye uwezekano wa kukamata dola 2015 kwa njia ya kura. Ni wazi hapa ndipo panapohitajika uwajibikaji na ushirikiano wa hali ya juu.Ningelikuwa mwanachama wa Chadema ningehakikisha katika uchaguzi wa ndani wa chama majabali hawa wawili hawaguswi. Wabaki kama walivyo. Wakamilishe kazi waliyoianza ambayo ni kukamata dola.Kisha baada ya hapo historia itakuwa imeandikwa.

No comments:

Post a Comment