Saturday, April 5, 2014

MTOTO WA AJABU JIJINI DAR...HIVI NDIVYO VITU VYA KUSHANGAZA ANAVYOWEZA KUVIFANYA

  
Mkazi wa Mbezi-Kibanda,  Andrea Marcus.
 AMA kweli ukistaajabu ya Musa utayaona ya Farao, Andrea Marcus (13), mkazi wa Mbezi-Kibanda cha Mkaa, Dar anadaiwa kuwa wa ajabu kutokana na vitendo vyake.
Mtoto huyu amedaiwa kuwa ni wa kichawi kutokana na maajabu yafuatayo: 
Ana uwezo wa kula ubwabwa sufuria moja la familia, anamudu kunywa maji ndoo moja, ana uwezo wa kuingiza tumboni mikate mikubwa saba kwa mlo mmoja,  amewahi kula mchele (si ubwabwa) ndoo nzima.
Mbaya zaidi baada ya kula milo hiyo huwa haoneshi ameshiba.

Maajabu mengine ambayo yanawashangaza watu wanaoishi naye ni jinsi anavyokula chakula kwa kumwaga chini kisha kukomba mpaka udongo.
“Sina amani ya moyo, naomba Watanzania wanisaidie, mwanangu ananiuma sana, hata kujisaidia ni hapohapo, chakula anakula kupita kiasi, kama nilivyosema hashibi na bado hali kama mwanadamu wa kawaida,” alisema mama wa mtoto huyo.
Akizungumzia madai ya uchawi, mama huyo, Angelina Marcus alisema mwaka 2001 alimzaa Andrea katika mimba ya miezi nane kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar.

“Nilipofika nyumbani tu, alikuja mwanamke mmoja, akasema amekuja kunipa hongera. Wakati anaingia alianguka, kichwa ndani miguu nje, alipoamka akaaga akisema anakwenda kuniletea kisamvu.
“Mama yangu akamwambia mzazi hali kisamvu, kama anataka akanichinjie bata. Yule mwanamke aliondoka, hakurudi tena,” alisema mama Andrea.

Aliendelea kudai kuwa, baada ya wiki tatu mtoto wake alianza tabia ya kulia usiku wa manane.
“Hiyo tabia ya kulia amekuwa nayo miaka yote, tulikwenda kwa waganga lakini wapi! Tukahamia makanisani kwa wachungaji kidogo mtoto alipata nafuu mwaka jana.
“Mwezi Novemba tarehe kumi na moja, mwaka jana (2013) yule mwanamke alikuja hapa nyumbani na kuniambia kuwa, mguu ule ni wangu.
“Alikaa chini mimi nikiwa nafua, akaanza kuniambia ‘mjukuu wangu samahani, nimeona unateseka sana na mwanao, nataka nikurudishie kwani mimi uchawi sasa basi.’

“Nilishtuka, nikamuuliza bibi unasema nini? Akajibu, ‘n imekuja kukwambia huyu si mtoto ni picha tu, mtoto wako ninaye mimi nyumbani kwangu na nina watoto wengi ila wa kwako ananisumbua, bora uje umchukue kesho asubuhi,” alisema mama Andrea.
“Siku iliyofuata nilikwenda kwake, sikumwona mtoto ila cha kushangaza aliniambia kuwa yeye anajua kuroga lakini hajui kutegua, ana mganga wake yupo Songea (Ruvuma), atampigia simu aje amtegue mtoto wangu arudi katika hali ya kawaida,” aliongeza mama Andrea.

Mama huyo alisema kuwa aliporudi nyumbani, aliwaambia wazazi wake kilichotokea na maneno yote waliyoongea na mwanamke huyo.
Wazazi wa mama Andrea walimuita mwanamke huyo akiwa na mumewe na mtoto wao mmoja, wakamuuliza kuhusu madai hayo, akaomba msamaha kwa kilichotokea. 

Sakata hilo likaenda Serikali ya Mtaa Misigani ambapo mwanamke huyo alikiri mara ya kwanza na kusema kuwa amempigia simu mganga wa Songea atafika wakati wowote.
“Cha kushangaza alikaa kwa nusu saa na kusema amewapigia simu ndugu zake wamesema huyo mganga amefariki dunia. Kila mtu alimuuliza amepigaje simu mbona wamekaa naye na hajatoka nje? Akanyamza,” alisema mama Andrea.
Mama Andrea alisema serikali ya mtaa waliliona sakata hilo ni kubwa na kuamuru babu wa Andrea (jina lipo) kuchukua barua kuipeleka kwenye Kata ili kesi ihamie huko. 

Mama huyo alimalizia kwa kusema kuwa anashindwa cha kuamua kwani kwa maelezo ya mwanamke huyo hajui akubali mtoto Andrea si wake au la!

No comments:

Post a Comment