Tuesday, April 22, 2014

MAREKANI YAPINGA UCHAGUZI WA RAIS SYRIA SABABU HIZI HAPA.


Rais wa Assad wa Syria.
Msemaji wa Ikulu ya White House ametaja uchaguzi wa Urais uliopangwa kufanywa nchini Syria kama "Mzaha wa Demokrasia".
Jay Carney alisema matokeo ya uchaguzi huo hayatatambuliwa nchini au nje.
Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Ulaya wametoa maoni sawa na hayo, na kusisitiza kuwa uchaguzi kama huo utavuruga utaratibu wa kisiasa nchini humo.
Mpango wa kimataifa wa kisiasa nchini humo unatarajia kuunda Serikali ya mpito ambayo itasimamia mambo hadi Uchaguzi huru utakapofanywa.
Lakini Rais Bashar al-Assad alisema hivi majuzi kuwa uhasama nchini humo umefikia kilele chake kwa sababu ya hatua muhimu zilizofaulu kijeshi dhidi ya waasi. Wachanganuzi wa maswala ya kisiasa wanasema kuwa angependa uchaguzi huo uthibitishe kuwa amethibiti utawala nchini humo.
Tangazo la uchaguzi limefanywa wakati ambapo habari zimepenyeza kuwa kemikali ya sumu imetumiwa katika mashambulizi mapya nchini humo.
Marekani inasema kuna ishara kuwa kemikali ya sumu, inayoshukiwa kuwa chlorine, ilitumiwa katika uwanja wa vita mwezi huu na inachunguza iwapo Serikali ya Syria ilihusika.
Hadi kufikia sasa Syria imetajwa kuondoa asilimia 65 ya silaha zake za kemikali kufuatia mapatano ya mwaka uliopita yaliyoafikiwa baada ya shambulio lililowaua watu wengi ambalo mataifa ya magharibi yalilaumu utawala wa Rais Assad.

No comments:

Post a Comment