Sunday, April 27, 2014

JAJI JOSEPH SINDE WARIOBA :MATUSI HAYATALETA KATIBA

 
 
Wakati matusi, dhihaka na kejeli dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, yakipamba moto ndani ya Bunge Maalum la Katiba, amewataka wajumbe hao kuacha malumbano na kuishambulia Tume na badala yake watafute maridhiano vinginevyo katiba mpya haitapatikana.
Warioba pia alionyesha kusikitishwa na kile kinachoendelea katika Bunge hilo kwa baadhi ya wajumbe wake kurushiana maneno wao kwa wao, huku wakitumia lugha ambazo hazina matumaini kwa ajili ya kufanikisha upatikanaji wa katiba mpya.
Alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuzindua ripoti maalumu iliyotolewa na Taasisi ya Utafiti ya Twaweza kuhusu Katiba, jana jijini Dar es Salaam.
Kutoakana na hilo, aliwataka wajumbe kujirekebisha kwa kujadili kwa kina rasimu ya katiba, ambayo ina maoni ya wananchi, kwani ndicho kilichowapeleka katika Bunge hilo.
“Tume ilipata maoni kutoka kwa wananchi wanaozungumzia utawala bora, wanataka kuwapo kwa miiko ya uongozi. Lazima uwazi, ukweli na uwajibikaji uthaminiwe. Wajirekebishe, wafanye kile ambacho wananchi wamewapeleka,” alisema Jaji Warioba.
Mbali na hilo, pia Warioba alieleza kuingiwa na wasiwasi wa kupatikana katiba mpya kutokana na namna ambavyo majadiliano yanaendelea bungeni kwa baadhi ya wajumbe kurushiana maneno ya kejeli ambayo hayalengi kufanikisha kazi hiyo kubwa ya taifa.
“Lugha wanayotumia hainipi matumaini ya kufanikiwa katika kazi waliyopelekwa hapo. Naomba wasiijadili tume, bali wajadili mambo ya msingi yaliyomo kwenye rasimu hiyo ambayo ni maoni ya wananchi. Yaliyomo kwenye rasimu siyo mali ya Tume, ni maoni ya wananchi.”
Aliwashauri wajumbe hao kufikia maridhiano kwa kuwa katiba haiwezi kupatikana bila ya kuwapo kwa muafaka baina yao.
Alisema Tume hiyo iliundwa na watu kutoka makundi na itikadi tofauti, lakini walifanikisha kazi ya kuzunguka sehemu mbalimbali nchini kukusanya maoni kutoka kwa wananchi na kuyaweka kwenye rasimu hiyo bila malumbano yoyote baina yao jambo ambalo linaonekana kuwapa shida wajumbe wa Bunge hilo.
“Ni lazima pawepo na maridhiano na makubaliano baina yao, lakini kwa hali hii ninayoiona ikiendelea, sijui kama watafanikiwa katika kazi hiyo,” alisema Jaji Warioba
Aliongeza: “Sisi tulikuwa na makundi mbalimbali, lakini hatukuwa na siasa katika kazi ya kukusanya maoni. Tulikuwa pamoja hadi kufanikisha kazi, Tume ilikuwa ya wananchi.”
Jaji Warioba alitoa kauli hiyo kufuatia mashambulizi makubwa yanayoendelea kutolewa dhidi yake na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyokuwa anaiongoza, kutoka kwa baadhi ya wanasiasa, wakiwamo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kwamba yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ni maoni ya Tume na siyo ya Watanzania.
Kwa upande wake, mjumbe wa Bunge la Katiba, ambaye pia ni Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangalla, alisema kujitoa kwa baadhi ya wajumbe kutoendelea na vikao, siyo sababu ya kuvunjika kwa Bunge hilo bali litavunjika lenyewe hapo baadaye iwapo safu inayotakiwa kikanuni itapungua.

No comments:

Post a Comment