Wajumbe wa Bunge la Katiba wakiwa wamesimama baada ya Mkiti Sitta ameahirisha kikao na Jaji Warioba kuondoka.
Hapa wajumbe wa Katiba wakiwa wamesimama kumzuia Jaji Warioba asiongee.
BARUA YA UMOJA WA KATIBA YA WANANCHI (UKAWA) KWA
MWENYEKITI WA BUNGE MAALUM, MHESHIMIWA SAMWEL J. SITTA,
KUHUSU UKIUKWAJI WA KANUNI ZA BUNGE MAALUM
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Sisi ambao majina yetu yameorodheshwa hapa chini ni Wajumbe wa Bunge Maalum ambao tunatokana na vyama vya CHADEMA, CUF, NCCR Mageuzi, DP, UDP, CHAUSTA, CHAUMA, NRA, NLD na CCK pamoja na Wajumbe walioteuliwa kutokana na makundi yaliyotajwa katika kifungu cha 22(1)(c) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83.
Tumeunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (‘UKAWA’) wenye lengo la kuhakikisha kwamba mchakato wa sasa wa Katiba katika Mkutano huu wa Bunge Maalum unapelekea nchi yetu kupata Katiba Mpya na bora kwa ajili ya nchi yetu.
Kwa sababu ya mwendelezo wa matukio ya ukiukwaji wa makusudi wa Kanuni za Bunge Maalum, 2014, ambao umefanyika
tangu ulipoapishwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum, kama tunavyoonyesha hapa, tunapenda kukufahamisha kwamba hatuko tayari kuendelea kukaa kimya wakati unaendelea kuvunja Kanuni za Bunge Maalum na kupelekea Mkutano wa Bunge Maalum kuwa hatarini kuvunjika.
Katika kipindi cha siku nne tangu umeapishwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum umefanya maamuzi yafuatayo yanayodhihirisha ukiukwaji wa Kanuni:
1. Tarehe 14 Machi, 2014, mara tu baada ya kuapishwa ulitangaza kwamba Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba atawasilisha Rasimu ya Katiba siku ya Jumatatu, yaani leo. Aidha, ulitangaza kwamba baada ya Mwenyekiti wa Tume kuwasilisha Rasimu, kutakuwa na kipindi cha siku tatu kwa Wajumbe wa Bunge Maalum kufanya mjadala wa jumla juu ya Rasimu kwa lengo la ‘kufungua vifua vyao.’
Vile vile, ulilitaarifu Bunge Maalum kwamba baada ya hapo Mheshimiwa Rais atakuja kulihutubia Bunge Maalum kati ya siku ya Jumanne au Jumatano.
2. Licha ya Wajumbe kadhaa wa Bunge Maalum kukuomba ubadilishe msimamo wako juu ya masuala haya, tarehe 15 Machi uliendeleza msimamo huo na ukaongeza kwamba Mwenyekiti wa Tume atawasilisha Rasimu ya Katiba kwa muda usiozidi dakika sitini na baada ya hapo kutakuwa na siku tatu za semina itakayoongozwa na wataalamu kutoka nje ya nchi yetu na baadaye ndiyo Mgeni Rasmi atakuja kulihutubia Bunge Maalum.
3. Leo tarehe 17 Machi baada ya malalamiko ya Wajumbe kadhaa umesema kwamba umeshauriana na Mwenyekiti wa Tume jana tarehe 16 Machi na mmekubaliana kwamba muda wa saa mbili (dakika mia moja ishirini) zitamtosha
Mwenyekiti wa Tume kuwasilisha Rasimu ya Katiba. Hii inathibitisha kwamba ulipopanga muda wa dakika sitini kwa ajili hiyo siku ya tarehe 15 Machi ulikuwa hujashauriana na Mwenyekiti wa Tume kama inavyotakiwa na Kanuni za Bunge Maalum.
Aidha, kwa taarifa tulizo nazo, inaelekea Mwenyekiti wa Tume analazimishwa kukubaliana na muda ambao wewe mwenyewe na nguvu nyingine zilizo ndani na nje ya Bunge Maalum mmempangia. Kwa maoni yetu, yote haya ni ukiukwaji wa makusudi wa Kanuni:
(a) Kanuni ya 7(1)(g) na (h) ya Kanuni za Bunge Maalum imeweka mpangilio wa shughuli zote za Bunge Maalum
ambapo ‘hotuba ya ufunguzi ya Mgeni Rasmi’, i.e., Rais wa Jamhuri ya Muungano au Rais wa Zanzibar, itafuatiwa na ‘uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba.’
Kwa jinsi ya mpangilio wa shughuli uliowekwa na Kanuni ya 7(1), uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba kabla ya hotuba ya ufunguzi ya Mgeni Rasmi ni ukiukwaji wa Kanuni za Bunge Maalum na, kwa vyovyote vile, kunatoa picha kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuja Bungeni kama mchangiaji wa hoja badala ya kuja
kama Mkuu wa Nchi kwa lengo la kufungua Bunge Maalum;
(b) Kanuni ya 47(a) inaelekeza kwamba “Mwenyekiti baada ya kushauriana na Mwenyekiti wa Tume watapanga muda unaofaa kwa ajili ya Mwenyekiti wa Tume kuwasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalum.”
Pamoja na kwamba kanuni hiyo imeanza kwa maneno ‘isipokuwa kama imeelezwa vinginevyo kwenye Kanuni hizi au Mwenyekiti ameelekeza vinginevyo’, ufahamu wetu wa Kanuni za Bunge Maalum unatuelekeza kwamba Mwenyekiti wa Bunge Maalum hana uwezo kikanuni wa kujipangia yeye mwenyewe muda ambao Mwenyekiti wa Tume atahitaji kwa ajili ya kuwasilisha Rasimu ya Katiba.
Muda huo unatakiwa kupangwa kwa pamoja baada ya mashauriano baina yao.
(c) Kwa mujibu wa kanuni ya 31(3), “baada ya Rasimu kuwasilishwa ... Mwenyekiti atatangaza majina ya wajumbe wa kila Kamati ... na kila Kamati itatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na Kanuni hizi.”
Aidha, kwa mujibu wa mpangilio wa kanuni ya 32, baada ya Kamati kuundwa, Rasimu itajadiliwa katika Kamati na baadaye katika Bunge Maalum. Kwa mtiririko wa Kanuni ulivyo, hakuna namna yoyote halali kwa Bunge Maalum kufanya semina ya wataalamu wa ndani au nje ya nchi kwa lengo la wajumbe kufungua vifua vyao au kwa lengo lingine lolote.
(d) Matumizi mabaya ya kanuni ya 85 inayohusu mamlaka ya kutengua kanuni. Ijapokuwa kanuni ya 85(1)
inatamka kwamba “... kanuni yoyote inaweza kutenguliwa kwa madhumuni mahsusi ...”, kanuni hiyo imefungwa na masharti ya kanuni ya 85(4) inayoelezea mazingira yanayoweza kusababisha kanuni itenguliwe.
Kwa kifupi, kanuni inaweza kutenguliwa kwa ajili ya kuahirisha kikao au kuongeza muda wa shughuli au kuongeza orodha ya shughuli yoyote ambayo haikuwepo kwenye mpangilio wa shughuli za siku hiyo. Nje ya mazingira hayo, Bunge Maalum haliwezi kutengua kanuni zake.
Kwa sababu ya ukiukwaji huu wa Kanuni za Bunge Maalum tunapenda kukujulisha kwamba sisi wanachama wa UKAWA hatuko tayari kuunga mkono, na tutapinga kwa kadri ya uwezo wetu mambo yafuatayo kufanyika ndani ya Ukumbi
wa Bunge Maalum:
(i) Uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba na Mwenyekiti wa Tume kabla ya hotuba ya ufunguzi wa Bunge Maalum na Rais wa Jamhuri ya Muungano au Rais
wa Zanzibar;
(ii) Semina yoyote itakayoongozwa na wataalamu wa ndani au nje ya nchi yetu kama ulivyolitangazia
Bunge Maalum;
(iii) Hotuba ya Mgeni Rasmi endapo itafuatia uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba;
(iv) Jambo lingine lolote linalokiuka Kanuni za Bunge Maalum.
Tunatarajia kwamba utayapa masuala haya tafakuri ya kutosha ili uweze kufanya maamuzi kwa kutumia Kanuni za Bunge Maalum. Tunaamini utatumia busara na hekima ili kuliepusha Taifa letu na fedheha ya vurugu zisizokuwa na sababu ndani ya Bunge Maalum.
Tunatanguliza shukrani zetu za dhati.
No comments:
Post a Comment