VIONGOZI wa Chama kipya cha siasa cha Alliance for Change and Transparency (ACT), juzi walijikuta wakizomewa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Mbugani, Jimbo la Nyamagani, jijini Mwanza.
Mbali ya kujikuta katika wakati mgumu wa kuzomewa, baada ya mkutano huo kumalizika, viongozi hao waliondolewa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Mkutano huo ulilenga kukitambulisha chama hicho ambacho bado hakijapata usajili wa kudumu. Viongozi waliokumbwa na kadhia hiyo ni Mwenyekiti wa muda wa ACT Taifa, Bw. Lucas Limbu, Katibu Mkuu wa muda, Bw. Samson Mwigamba na Bw. Willy Mushumbusi (Katibu wa chama hicho jijini Mwanza).
Viongozi hao walizomewa na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambao walihudhuria mkutano huo baada ya viongozi hao kukishambulia chama chao.
Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Misungwi, mkoani humo, Jane Kajoki ambaye mwaka 2010 aligombea ubunge jimbo hilo kwa tiketi ya CHADEMA, alisema lengo la kuanzisha chama kipya ni kumkomboa Mtanzania maskini.
Malengo mengine ni kusimamia haki ya kila mwananchi ambaye anapaswa kushiriki katika maamuzi ya nchi yake na kuongeza kuwa, chama hicho kimepata udhamini wa wanachama 200 kila Mkoa ili kiweze kupata usajili wa kudumu ambao utakiwezesha kiweze kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Wakati akiendelea kusalimia wananchi na kukishambulia CHADEMA, Kajoki naye a ijikuta akizomewa na kuambiwa msaliti ambapo pamoja na kuwasihi wananchi, wamsikilize jitihada hizo zilionekana kugonga mwamba wakionesha alama ya vidole viwili ambayo hutumiwa na CHADEMA.
Wakati Bw.Limbua kihutubia wananchi, alikishambulia CHADEMA na kujikuta akizomewa na wafuasi wa chama hicho ambao walishiriki mkutano huo.
Bw.Limbu aliwafananisha wafuasi wa chama hicho sawa na mbwa waliotumwa kwenda kuwazomea ambapo hali ya kuzomea, pia ilimkuta Bw. Mwigamba ambapo wakati akihutubia, wafuasi hao walionesha alama ya vidole viwili kila alipoeleza udhaifu wa viongozi wa CHADEMA na kukiponda chama hicho.
Wakiwa jukwaani kwa nyakati tofauti, Bw.Limbu na Bw.Mwigamba, walionekana kuchochea hasira za wafuasi hao baada ya kuifananisha CHADEMA na CCM sawa na nguruwe pori.
Bw. Mwigamba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, mkoani Arusha, alisema chama hicho kikichukua nchi, kitaongoza kidikteta na kuongeza kuwa; “Mliotumwa kuja kuzomea mnabweka kama mbwa, kwa vile mnatuzomea, nasi tunajiandaa kuwazomea viongozi wenu mahali popote,” alisema Bw.Mwigamba.
Alisema baadhi ya vyama vimeanzishwa na kuendeshwa kama kampuni za watubinafsi, kufukuza watu kabla hakijashika madaraka sasa kikichukua nchi hali itakuwaje.
Aliwaomba wananchi kukiunga mkono chama chao ambacho kinatajwa kuanzishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw.Zitto Kabwe, baada ya kuvuliwa nyadhifa za uongozi ndani ya CHADEMA na kusisitiza kuwa, dhamira yao ni kukuza demokrasia shirikishi na Serikali inayowajibika.
Kabla ya mkutano huo, viongozi wa chama hicho walifanya uzinduzi wa baadhi ya matawi katika Kata ya Igoma, nje kidogo ya jiji hilo.
No comments:
Post a Comment