Kalenga. Padri wa Makanisa ya
Orthodox katika Kijiji cha Nyamihuu, Kata ya Nzihi, jimboni Kalenga
Constantino Mbilinyi (36) amepigwa na kujeruhiwa na watu wanaodaiwa kuwa
ni wafuasi wa CCM.
Baada ya kukutwa na mkasa huo, Padri Mbilinyi
alishikiliwa kwa muda katika Ofisi ya Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho,
Kumbusho Chengula, na baadaye alichukuliwa na askari ambao walimpeleka
Kituo cha Polisi Kati, mjini Iringa kwa mahojiano.
Kasisi huyo akizungumza na waandishi wa habari
jana alisema alipatwa na mkasa huo alipoambatana na viongozi wa Chadema
waliopiga kambi kwenye Kata ya Nzihi, ambao walikuwa wakielekea kwenye
mikutano ya kampeni za kumnadi mgombea ubunge kupitia chama hicho, Grace
Tendega.
Alisema viongozi hao walimwomba awasindikize
kwenda Kijiji cha Igangimali kwa ajili ya kumwona mtu aitwaye, Samti
Ngonjela ili wamkabidhi mabango Tendega.
“Waliniomba na mimi nikakubali kwa kuwa nilikuwa
na ratiba ya kwenda katika kijiji kile kumwona Bento Ngaila ambaye
tulitaka kuzungumza kuhusiana na mchakato wa shamba langu lililoko
katika kijiji kile,” alisema Mbilinyi na kuongeza:
“Tulipofika nilimtafuta Ngonjela kwa ajili ya
kuwaonyesha viongozi wa Chadema, lakini wakati huo vijana wengine wa
Chadema walianza kubandika mabango ya mgombea katika klabu ya pombe ya
Lazaro Nzigi, na ghafla lilitokea kundi la wanachama wa CCM na kuanza
kuwafukuza.”
Alisema vijana hao walimgeukia wakimshutumu kwamba
aliwapeleka watu wa Chadema katika eneo lile ambalo wao walikuwa na
mkutano wa ndani.
Mbilinyi alisema licha ya kujitetea, wafuasi hao
wa CCM walimkamata na kumwangusha na kumfunga mikono nyuma kwa kamba ya
katani. Wakati huo wafuasi wa Chadema walikuwa wameshaondoka.
“Walianza kunipiga na kunisukuma hali iliyonifanya
nianguke chini na kuumia mkononi na mgongoni. Nikiwa nimeanguka chini
na mikono yangu imefungwa kamba kwa nyuma mmoja wa vijana hao alichukua
pilipili na kuingiza kwenye mfuko wa shati langu kisha wakanichukua na
kunipeleka ofisi ya ofisa mtendaji iliyoko Nyamihuu,” alisema Mbilinyi.
Mbilinyi alisema makada hao wa CCM walimweleza
ofisa huyo kwamba alikwenda na wenzake kuwafanyia fujo na kwamba
aliwatukana na kuwatishia maisha. Alisema watu waliomfanyia unyama huo
anawafahamu.
Ofisa Mtendaji
Kaimu Ofisa Mtendaji, Chengula alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa alilazimika kumweka ndani kwa
kuhofia hali ya usalama.
No comments:
Post a Comment