Friday, March 28, 2014

ROBERT MUGABE KUSUSIA MKUTANO UMOJA WA ULAYA ENDAPO MKEWE HATAALIKWA



Serikali ya Zimbabwe imeeleza kuwa rais Robert Mugabe ataususia mkutano uliopangwa kufanyika mwanzoni mwa April kati ya Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Ulaya (EU) endapo mkewe Grace hataalikwa.
Mkutano huo utafanyika Brussels, Ubeligiji (katika bara la Ulaya) ikizingatiwa kuwa mwaka 2002 Umoja wa Ulaya uliwawekea vizuizi Robert Mugabe na mkewe Grace kutozitembelea nchi za bara la Ulaya.
Mugabe ambaye ni makamo mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) amepewa mualiko wa kuhudhuria mkutano huo lakini mkewe hakupewa mualiko huo.
Balozi wa EU nchini Zimbwabwe, Aldo Dell’Ariccia alieleza wiki iliyopita kuwa Umoja huo wa Ulaya unawaalika kwenye mkutano watu ambao wana kazi ya kufanya kwenye mkutano huo na kwamba program za kikao hicho hazihusishi wana ndoa.
Kauli ya balozi huyo ilionekana kumkera Mugabe na msemaji wake akarudisha mashambulizi kwa mshangao.
“Ni kitu cha kushangaza kwamba EU haikutoa mualiko kwa First Lady. Kitu ambacho Mungu amekiweka pamoja EU inataka kukitenga. Hivi wanatarajia rais aiheshimu EU na kuikosea heshima ndoa yake mwenyewe?” alikaririwa msemaji wa Mugabe, George Charamba.
Mke wa Mugabe alikuwa akikosolewa kuwa hutumia pesa nyingi kufanya manunuzi ya anasa kila anapolitembelea bara la Ulaya.

No comments:

Post a Comment