Sunday, March 9, 2014

MBOWE AKERWA NA TABIA YA BAAZI YA WAJUMBE WA BUNGE LA KATIBA


       Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe,amekemea vikali tabia ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba,kuzomeana. Mbowe alisema kwa hali ilipofikia, kuna haja kwa kila chama kuwapa semina wajumbe wake, ili walione Bunge hilo kuwa ni la kitaifa na siyo kikao cha chama cha siasa. “Kuzomeana ni mambo ya kitoto, siwezi kupongeza utovu wa hali ya juu wa nidhamu ulioonyeshwa na baadhi ya wajumbe. Tukiruhusu zomeazomea, itakuwa sawa na genge la wahuni,” alisema Mbowe. Mbowe ambaye pia ni mjumbe wa Bunge hilo alisema, kuna mambo ya msingi yanapingwa tu kwa sababu yametolewa na mjumbe kutoka chama fulani cha siasa bila kuangalia mantiki ya hoja. “Ni kweli kiti kinayumba nafasi ya kuchangia inatolewa kwa upendeleo,lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya sisi kushindwa kuheshimiana na kuheshimu mawazo ya wengine,”alisema Mbowe na kuongeza;
“Kuna umuhimu wa vyama vyetu kurudi na kukaa na wajumbe wetu kwa sababu mvutano mkubwa hauko kwenye lile kundi la watu 201 ni vyama vya siasa,”alisema. Kwa mujibu wa Mbowe,kama Bunge hilo halitatunga kanuni kali ili kila mjumbe aheshimu mawazo ya wenzake na kuruhusu kila mjumbe, aseme bila utaratibu ni vurugu. Mbowe alisema kinachotokea ndani ya Bunge hilo kwa baadhi ya wajumbe kufanya mambo aliyoyaita ni ya kitoto ikiwamo kuzomea, ni kujidhalilisha na kushusha hadhi ya chombo hicho muhimu
Mjema D. / Mwananchi

No comments:

Post a Comment