Saturday, March 15, 2014

MAISHA PLUS KURUDI TENA HEWANI


Baada ya kusimamishwa kwa takriban wiki moja, vipindi vya Televisheni vya shindano la Maisha Plus, vinatarajiwa kurudi tena hewani leo saa tatu usiku, kupitia kituo cha televisheni kile kile, TBC1.
Akizungumza mapema asubuhi hii katika mkutano na wanahabari, Mratibu wa shindano hilo ambalo mwaka huu limepewa jina la Maisha Plus Rekebisha, Ally Masoud `Kipanya', amesema baada ya kukaa chini na uongozi wa televisheni hiyo, wamekubaliana kimsingi kutangaza ratiba itakayokuwa rasmi ambayo haitabadilika kama ilivyokuwa awali.
Uongozi wa Maisha Plus ulilazimika kusitisha matangazo ya kipindi hicho kutokana na kutokuwa na ratiba ya kueleweka ya vipindi hivyo na kusababisha wapenzi wa kipindi hicho kukosa muda maalum wa kuona matangazo.
Kipanya amesema ratiba ya vipindi itaanza upya na ratiba itakuwa kwamba, siku za ijumaa na jumamosi, vipindi vitaoneshwa kuanzia saa tatu usiku lakini siku zote za wiki zilizobaki, kipindi kitakuwa kinaruka saa nne na dakika tano usiku.
Alisema vipindi hivyo vitaonyesha hatua za awali ambazo ni usaili na mpaka kupatikana kwa washiriki 30 waliobahatika kuingia kijijini.
“Tutaanza kuwaonyesha kipindi chetu kuanzia leo hii saa tatu usiku, kipindi kitaanza kwa kuonyesha hatua za mwanzo kabisa za mashindano haya,” alisema Kipanya.
Alifafanua akisema kuwa vipindi 10 vya mwanzo vitaonyesha mchakato mzima wa upatikanaji wa vijana 18 kutoka Tanzania watakao ungana na vijana wengine 12 kutoka Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi zitakazotoa washiriki watatu kwa kila nchi.
Usaili wa mwaka huu ulikuwa tofauti na miaka mingine ambapo orodha ya washiriki 40 ilitengenezwa na ikagawanywa katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza lilikwenda mkoani iringa kuishi kwenye vijiji vya huko na kushiriki shughuli za kijamii.
Kundi la Pili litaenda visiwani Zanzibar ambalo pia litashiriki utamaduni wa kila siku wa kimaisha wa visiwani humo ambapo ni washiriki tisa tu katika kila kundi watachukuliwa na watachujwa kutokana na jinsi walivyoyamudu maisha ya huko.
“Vijana wakiwa huko katika vijiji vya kweli watakuwa wakishiriki shughuli za kilimo, usafi, za kiafya na nyinginezo kabla hawajaingia katika kijiji cha Maisha Plus”, alifafanua Kipanya.
Baada ya kundi la kwanza na la pili kutoa washiriki tisa kila kundi, washiriki 18 watakuwa wameshapatikana, na sasa nchi za zikishapata washiriki wake 12, idadi ya washiriki 30 itaingia kijijini cha Maisha Plus katikati ya mwezi huu.

No comments:

Post a Comment