Monday, March 31, 2014

HAYA NDIO MAKUNDI YA SANAA YALIYOPIGWA STOP NA BASATA KUTOA BURUDANI KATIKA MISS TANZANIA!



BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata), limeitaka Kamati ya Miss Tanzania kutohusisha burudani zinazokiuka maadili ya Mtanzania wakati wa mashindano yao mwaka huu.
Akizungumza wakati wa kikao cha tathmini ya mashindano ya Miss Tanzania 2013 kilichofanyika kwenye ukumbi wa baraza hilo, Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Idaya ya Ukuzaji Sanaa Basata, Vivian Shalua, alisema kuwa, maadili ni muhimu kuzingatiwa katika mashindano hayo ili kuepukana na dhana potofu kuwa, yanahusiana na uhuni.
“Maadili yazingatiwe katika mashindano ya mwaka huu, kuanzia kwa washiriki hadi burudani zitakazohusishwa, kama ‘vigodoro’, ‘kanga moja mbendembende’ na nasikia siku hizi kuna ‘tisheti ndembendembe’,” alisema mkurugenzi huyo.

Alisema kuwa, Basata ipo tayari kuyapigania mashindano ya Miss Tanzania kuhakikisha yanakuwa katika ubora wa hali ya juu, kwa kushirikiana na Kampuni ya Lino International Agency ambao ndio waandaaji.

Mkurugenzi huyo pia aliitaka Lino kuwaelimisha mawakala wanaoandaa mashindano hayo juu ya umuhimu wa kuwa na vibali kutoka Basata, ikiwa ni pamoja na kutowavumilia watovu wa nidhamu bila kujali ukongwe wao katika tasnia hiyo.
Kwa upande wake, Ofisa Sanaa Kitengo cha Matukio, Kurwijira Maregesi, aliitaka Lino kujipanga kujiweka tayari kufanya mashindano hata pale inapokosa mdhamini, huku mjumbe mwingine katika kikao hicho, ambaye ni Ofisa Sanaa Basata, Philemon Mwasanga, akisisitiza mawakala kuwekeana mikataba na warembo kabla ya mashindano kuanza.

“Lino isiwafumbie macho mawakala wasiojali mikataba na warembo, na warembo waisome na kuielewa ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea,” alisema.

Akijibu hoja kadhaa zilizoibuliwa katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Lino International Agency, Hashimu Lundenga, alisema kuwa, wamejipanga ili kuweza kufanya mashindano yao bila kutegemea wadhamini, huku akiitaka Basata kuwasaidia katika hilo.

“Tatizo mashindano yetu gharama yake ni kubwa sana, nasi hatupendi kuona ubora wake ukishuka kutokana na kushindwa kumudu gharama, ndio maana tumekuwa tukihangaika kuomba udhamini kutoka katika makampuni mbalimbali makubwa hapa nchini,” alisema.
Juu ya mikataba baina ya warembo na mawakala, Lundenga alisema: “Mwaka huu tumesisitiza mawakala waingie mikataba na washiriki kabla ya mashindano na tutakuwa makini katika kufuatilia hilo na changamoto nyinginezo zilizoibuliwa katika kikao hiki.”
Mmoja wa warembo walioshiriki mashindano ya mwaka jana ambaye ni Miss Sinza 2013, Prisca Clement, alisema kuwa, kuna umuhimu wa kuongezwa kwa zawadi katika ngazi za chini ili kumwezesha mshiriki kujivunia na kujitosa kwake katika mashindano hayo bila kujali kama ameshinda au la.
Mashindano ya Miss Tanzania 2014 yamezinduliwa mapema wiki hii, ambapo fainali zake zinatarajiwa kuwa kati ya Septemba na Novemba mwaka huu chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Redd’s Original.

No comments:

Post a Comment