DK. SLAA AIBUA MAPYA IPTL
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Wilibrod Slaa, amesema fedha zilizochotwa katika Akaunti ya Tegeta
Escrow ni sh bilion 400 badala sh bilioni 306 kama ilivyokaririwa na
vyombo vya habari kutoka bungeni.
Hayo
aliyabainisha juzi na Katibu Mkuu huyo katika mkutano wa hadhara wa
kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika katika mtaa wa
Mnazi mmoja Manzese, Tip top jijini Dar es Salaam.
Dk. Slaa alisema kutokana na tuhuma hizo, alifuatilia bunge hatua kwa
hatua hadi likaisha kwa maridhiano, akiamini wezi wa fedha hizo
watachukuliwa hatua lakini cha kushangaza hadi leo hawajachukuliwa hatua
nab ado wanaendelea na kazi.
“Fedha alizochukua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Prof. Anna Tibaijuka na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter
Muhongo ni ukweli uliowazi kuwa Rais Jakaya Kikwete anajua na ndio maana
mawaziri hao wamekuwa na jeuri.
“Suala la Escrow ni bichi kuliko mnavyofikiria, lugha ya Mwalimu
Nyerere aliposema watu wanaokimbilia Ikulu tuwaogope kama ukoma, Ikulu
ni mahali patakatifu mahali pa heshima kumbe wakubwa walijua kuna nini?
Atoke Kikwete hadharani kama nasema uongo,” alisema.
Alisema hajawahi kuona Waziri dhaifu kama Waziri Mkuu Mizengo Pinda
kwani kama angekuwa makini, angeweza kuzuia wizi huo usitokee.
“Mfumo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni mbovu kuanzia Kikwete mwenyewe
na serikali za mitaa hata wabadilishwe viongozi katika chama hicho bado
hakutakuwa na mabadiliko ya kimaendeleo nchini,” alisema Dk. Slaa.
Naye Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe alisema kuwa nguvu ya
CHADEMA ya kusimamisha wagombea katika mitaa na vitongoji kwa asilimia
98 katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini imewatia hofu CCM.
Mbowe, alisema baada ya kubaini mbinu chafu za chama hicho,
kuwawekea wagombea wa CHADEMA pingamizi huku wengine wakienguliwa
kimizengwe ni dalili ya wazi kwamba chama hicho kinahofu ya kushindwa.
“Presha hiyo inawafanya wawaengue wagombea wetu kwa kuwajengea hoja
zisizo na msingi mara utasikia jina limekosewa mara sijui jina la chama
liko hivi ili mradi tu wakipunguze nguvu chama chetu.
“Nawaomba wakazi wa Vijibweni ikifika Desemba 14 siku ambayo itakuwa
ya uchaguzi, mjitokeze kwa wingi kama mlivyojitokeza leo ili mkawapigie
kura wagombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA),” alisema Mbowe.
Mbowe, alisema CHADEMA haitaki ushindi wa dezo bali wanataka uchaguzi
huru na wa haki ili mshindi atakayepatikana, ashinde kwa haki.
Aidha, CHADEMA imetahadharisha kuwa endapo vurugu za kuwaengua
wagombea wake zitaendelea, chama hicho kitakwenda mahakamani kusimamisha
uchaguzi huo.
Naye Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Temeke, Issaya Mwita, awali
akitoa taarifa ya mchakato wa uchaguzi huo alisema katika Kata hiyo ya
Vijibweni kuna mitaa sita.
Alisema katika mitaa hiyo, Chama Cha Wananchi (CUF), kimesimamisha wagombea wawili huku CHADEMA kikisimamisha wanne.
(CHANZO: TANZANIA DAIMA)
No comments:
Post a Comment