Pages

Saturday, December 6, 2014

DR SLAA! ASEMA FEDHA ZA ESCROW NI SH BILIONI 400 BADALA YA SH BILIONI 306

DK. SLAA AIBUA MAPYA IPTL

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilibrod Slaa.

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilibrod Slaa, amesema fedha zilizochotwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow ni sh bilion 400 badala sh bilioni 306 kama ilivyokaririwa na vyombo vya habari kutoka bungeni.
 
Hayo aliyabainisha juzi na Katibu Mkuu huyo katika mkutano wa hadhara wa kampeni za Uchaguzi wa Serikali  za Mitaa uliofanyika katika mtaa wa Mnazi mmoja Manzese, Tip top jijini Dar es Salaam.
Dk. Slaa alisema kutokana na tuhuma hizo, alifuatilia bunge hatua kwa hatua hadi likaisha kwa maridhiano, akiamini wezi wa fedha hizo watachukuliwa hatua lakini cha kushangaza hadi leo hawajachukuliwa hatua nab ado wanaendelea na kazi.
“Fedha alizochukua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo ni ukweli uliowazi kuwa Rais Jakaya Kikwete anajua na ndio maana mawaziri hao wamekuwa na jeuri.
“Suala la Escrow ni bichi kuliko mnavyofikiria, lugha ya Mwalimu Nyerere aliposema watu wanaokimbilia Ikulu tuwaogope kama ukoma, Ikulu ni mahali patakatifu mahali pa heshima kumbe wakubwa walijua kuna nini? Atoke Kikwete hadharani kama nasema uongo,” alisema.
Alisema hajawahi kuona Waziri dhaifu kama Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwani kama angekuwa makini, angeweza kuzuia wizi huo usitokee.
“Mfumo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni mbovu kuanzia Kikwete mwenyewe na serikali za mitaa hata wabadilishwe viongozi katika chama hicho bado hakutakuwa na mabadiliko ya kimaendeleo nchini,” alisema Dk. Slaa.
Naye Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe alisema kuwa nguvu ya CHADEMA ya kusimamisha wagombea katika mitaa na vitongoji kwa asilimia 98 katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini imewatia hofu CCM.
Mbowe, alisema  baada ya kubaini mbinu chafu za chama hicho, kuwawekea wagombea wa CHADEMA pingamizi huku wengine wakienguliwa kimizengwe ni dalili ya wazi kwamba chama hicho kinahofu ya kushindwa.
“Presha hiyo inawafanya wawaengue wagombea wetu kwa kuwajengea hoja zisizo na msingi mara utasikia jina limekosewa mara sijui jina la chama liko hivi ili mradi tu wakipunguze nguvu chama chetu.
“Nawaomba wakazi wa Vijibweni ikifika Desemba 14 siku ambayo itakuwa ya uchaguzi, mjitokeze kwa wingi kama mlivyojitokeza leo ili mkawapigie kura wagombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA),” alisema Mbowe.
Mbowe, alisema CHADEMA haitaki ushindi wa dezo bali wanataka uchaguzi huru na wa haki ili mshindi atakayepatikana, ashinde kwa haki.
Aidha, CHADEMA imetahadharisha kuwa endapo vurugu za kuwaengua wagombea wake zitaendelea, chama hicho kitakwenda mahakamani kusimamisha uchaguzi huo.
Naye Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Temeke, Issaya Mwita, awali akitoa taarifa ya mchakato wa uchaguzi huo alisema katika Kata hiyo ya Vijibweni kuna mitaa sita.
Alisema katika mitaa hiyo, Chama Cha Wananchi (CUF), kimesimamisha wagombea wawili huku CHADEMA kikisimamisha wanne.
(CHANZO: TANZANIA DAIMA)

No comments:

Post a Comment