Leo Jumamosi 05 Aprili 2014 ni siku ya mwisho ya kampeni za uchaguzi
mdogo wa Jimbo la Chalinze na kesho Jumapili 06 Aprili 2014 ni siku ya
wananchi kupiga kura.
Kwa wananchi wa Jimbo la Chalinze wa kata mbalimbali mnaoweza kupata
ujumbe kwa njia ya mtandao nawajulisha kwamba nitazungumza nanyi katika
mkutano wa hadhara leo.
Kampeni za Chalinze zilizinduliwa na Katibu Mkuu Dr. Wilbroad Slaa na
zitafungwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Said Issa Mohamed (ZNZ)
akiwa na Dr. Slaa.
Kwa wapenda demokrasia na maendeleo popote mlipo ziungeni mkono timu za
viongozi, wanachama na wapenzi kwenye kata na vijiji mbalimbali.
Wasiokuwa na mtandao naamini timu zetu za kampeni ya chini kwa chini na
zenye magari ya matangazo kwa pamoja zitakuwa zimeshawaalika kwa
kuzingatia ratiba ya kampeni. Tutahutubia kufunga kampeni kupitia
mkutano utakaofanyika eneo la Chalinze Mjini (Sokoni) kuanzia saa 8
mchana mpaka 12 jioni, nitakuwepo pamoja na viongozi wengine wa kitaifa.
Naandika ujumbe huu kwa wananchi wa Chalinze walio nje ya jimbo hilo
katika wilaya za jirani kufanya kila linalowezekana kurejea kwenda
kupiga kura ama walau muwasiliane na ndugu, jamaa na marafiki walio
katika kata na vijiji mbalimbali kujitokeza kupiga kura kesho na
kuchagua mabadiliko.
Huu ni zaidi ya uchaguzi, ni uchaguzi kati ya wanyonge na wenye mamlaka,
ni uchaguzi kati ya wakataa usultani na wakumbatia usultani, ni
uchaguzi kati ya walioshindwa kuboresha huduma na kuanza kutoa ahadi
nyingine za kilaghai dhidi ya wanaozijua shida na kero na walio tayari
kuzitatua. Ni uchaguzi wa kukataa ghiliba.
Kesho ni kwenda kupiga kura kwa CHADEMA kwa lengo la muda mfupi la
kuongeza mbunge mwingine wa upinzani na kupunguza hodhi ya chama kimoja
bungeni kuongeza nguvu yetu ya kuwakilisha wananchi na kuisimamia
Serikali.
Kesho ni kwenda kupiga kura za ushindi kwa CHADEMA kuipunguzia kura CCM
kwa lengo la muda wa kati la kuiondoa CCM madarakani katika chaguzi
zijazo kwa kuikataa kuanzia sasa ili kuleta uongozi bora, sera sahihi na
mikakati makini kwa maendeleo endelevu ya nchi yetu na wananchi wake.
Sababu zipo nyingi; nieleze chache na zingine nitazieleza mkutanoni. CCM
imekuwa ikitoa ahadi lukuki lakini utekelezaji ni kiduchu:
Mosi, Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005 kupitia ahadi za papo kwa papo na
Ilani ya Uchaguzi ya CCM alitoa ahadi nyingi kwa Chalinze na nchi nzima
kwa ujumla. Kati ya ahadi hizo ni pamoja na ile ya ‘maisha bora kwa kila
mtanzania’ ambayo utekelezaji wake umefanyika kinyume chake kwa
kuwaongezea mzigo mkubwa wa gharama na ugumu wa maisha kwa wananchi.
Kazi ya mbunge ni kuisimamia serikali kuwezesha maendeleo. Hivyo
Chalinze chagueni Mbunge kupitia CHADEMA Mathayo Torongey kwa kuwa
atakuwa huru ‘kuibana’ Serikali inayoongozwa na Rais Kikwete kuliko
mbunge wa CCM.
Pili, “Mabadiliko ya Kweli hayawezi kuletwa na mafisadi wale wale wa
chama kile kile kile chenye uoza ule ule, wakiendeleza yale yale; eti
kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya. Kwa falsafa ya chukua chako
mapema, Tanzania yenye neema haiwezekani”, hii ni nukuu kutoka Ilani ya
Uchaguzi ya CHADEMA ya mwaka 2005 kwenye sera yake ya ‘mfumo mpya wa
utawala’.
Wakati wa uchaguzi huo mapambano dhidi ya mafisadi hayakuibua mjadala
mkubwa wa kitaifa, hata hivyo madai mengi ya wakati huo yakadhihirika
tarehe 15 Septemba 2007 kupitia orodha ya mafisadi. Ikumbukwe kwamba
tarehe 16 Disemba 1959, Mwalimu Nyerere alitangaza maadui watatu wa
taifa ambao ni umaskini, ujinga na maradhi.
Tarehe 17 Mei 1960 alitoa kauli bungeni ya kuongeza adui mwingine mkubwa
zaidi na namnukuu: “Napenda kuongeza adui mwingine katika orodha ya
maadui wanaoitesa jamii yetu, ambao ni umaskini, ujinga na maradhi. Kwa
hakika, tunaweza kufanya juhudi za kushughulikia tatizo la umaskini.
“Tunaweza kufanya juhudi za kushughulikia tatizo la ujinga, pia tunaweza
kufanya juhudi za kushughulikia tatizo la maradhi. Lakini juhudi hizo
hazitazaa matunda endapo wananchi hawatakuwa na imani na Serikali yao.
Endapo hawatakuwa na imani na uadilifu wa viongozi watakaopewa madaraka
na Serikali, kutokana na viongozi hao kuwa ni wala rushwa.
"Lazima niwe mkweli. Nasema kwamba rushwa ipo. Kwa hiyo, Mhe. Spika,
lazima rushwa ipigwe vita sana kwa sababu naamini kuwa; rushwa ni adui
anayeleta madhara makubwa zaidi kwa wananchi wakati wa amani, kuliko
madhara yanayosababishwa na vita wakati wa vita. Mimi naona kuwa, kosa
la rushwa linastahili kuwekwa katika kiwango kilicho sawa na kosa la
uhaini, kwa sababu linaondoa kabisa imani ya wananchi kwa Serikali
yako”.
Kwa wosia huo wa Mwalimu Nyerere kuichagua CCM ambayo imehusishwa na
ufisadi wa Fedha za Malipo ya Akaunti ya Nje (EPA) kupitia kampuni ya
Kagoda na ufisadi mwingine mwingi kwa nyakati mbalimbali ni kumkumbatia
adui mwenye madhara kuliko vita.
Adhabu ya uhaini huwa ni kifungo kirefu au hata kifo, kwa maneno ya
Mwalimu Nyerere mafisadi wanastahili adhabu sawa na wahaini; kifo au
kifungo cha mafisadi wa kisiasa ni kuwakataa katika sanduku la kura.
Hivyo, hata bila kujali CHADEMA imemsimamisha mgombea gani; wananchi wa
Chalinze wanapaswa kuacha kuipa kura CCM na kuchagua CHADEMA ambayo
imeonyesha dira na dhamira katika dhima yake ya kupambana na ufisadi.
Uadilifu wa Mathayo Torongey ni mkubwa kuliko wa Ridhwani Kikwete, hivyo
ili kusimamia vizuri rasilimali za umma katika Halmashauri na Bungeni
kuchangia katika maendeleo ya Chalinze na Taifa. Hivyo, leo tuungane
kutafuta kura za CHADEMA kesho zipigwe na tuzilinde kuwezesha
mabadiliko.
Tatu, CHADEMA ni chama chenye sera mbadala kinachopaswa kupigiwa kura na wananchi kiongeze nguvu za kuzisimamia.
Sikuwa na mpango wa kuja Chalinze kwenye kampeni kwa kuamini kwamba
viongozi wenzangu walio nje ya Bunge Maalum wanatosha kumaliza kampeni.
Hata hivyo, yanayojiri katika Bunge Maalum yamenifanya niamue kutumia
fursa hii ya kampeni kufikisha ujumbe kwa wananchi na kuhamasisha
mabadiliko.
Itakumbukwa kuwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 CHADEMA
kiliahidi kuanzisha mchakato wa katiba mpya ndani ya Siku 90/100 za
utawala.
Pamoja na kuwa hakikutangazwa kuingia madarakani kiliamua kusimamia sera
hiyo kwa wabunge kususia hotuba ya Rais Kikwete bungeni, kutangaza
kutoyatambua matokeo ya urais na kushinikiza mchakato wa kuandika katiba
mpya uanze. Ndani ya siku 100 Rais Kikwete akatangaza kuanzisha
mchakato.
Hata hivyo, kwa kuwa hakukuwa na dhamira njema ndani ya Serikali na CCM
toka kuanza kwa mchakato huo kumekuwa kukitungwa sheria mbovu mbovu
zenye kuchelewesha na ‘kuchakachua’ mchakato katika hatua mbalimbali.
Katika hatua ya sasa Rais ametumia vibaya madaraka makubwa aliyokuwa
amepewa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kuteua viongozi, makada na
mawakala wengi wa CCM miongoni mwa wajumbe 201 wa Bunge Maalum.
Hatimaye akalihutubia Bunge Maalum na kwenda kinyume kabisa na misingi
muhimu ya rasimu ya katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
Izingatiwe kwamba Rais angeweza kutoa maoni yake rasimu ya kwanza
ilipotolewa, hakufanya hivyo na kuamua kwenda kupinga rasimu ambayo
imewasilishwa Bungeni kwa maelekezo yake. Rais amesababisha kwamba
katika Kamati za Bunge Maalum wajumbe wengi wanaotokana na chama chake
au aliowateua wanamtumia yeye kama rejea badala ya ripoti za maoni ya
wananchi na utafiti wa wataalamu.
Pamoja na ‘kuchakachua’ rasimu ya katiba kuondoa muundo wa Muungano wa
Shirikisho la Serikali tatu na kuingiza muundo ule ule wa Serikali mbili
kama ilivyo katika Katiba ya mwaka 1977. Wajumbe hao wamefikia hatua
hata ya kupiga kura ya ibara za rasimu wakitaka hata masuala mengine
kwenye tunu za taifa mathalani uzalendo, uwazi na uwajibikaji
yaondolewe.
Kura za wajumbe kufikisha theluthi mbili (2/3) kuwezesha ‘uchakachuaji’
huo hazikutokana na uteuzi tu bali pia zinatafutwa kwa njia nyingie za
vitisho na za kifisadi. Katika hali ya sasa sioni dalili za mchakato huu
kusonga mbele, utakwamia katika mjadala wa sura ya kwanza na sura ya
sita.
Mjadala huu utaibuka katika Bunge la Bajeti ambapo mbunge mpya wa
Chalinze atakuwa amepatikana. Naomba wananchi mumchague Mathayo Torongey
CHADEMA tupate mbunge mwingine ili ukija mjadala wa muswada mwingine wa
sheria unaohusiana na sheria ya mabadiliko ya katiba au kura ya maoni
kuwe na sauti nyingine ya kuisimamia Serikali.
Tusitarajie kwamba Ridhwani ataweza kupinga miswada mibovu inayoletwa
bungeni baada ya kupitishwa na baraza la mawaziri chini ya uenyekiti wa
Rais Kikwete. Huu ni uchaguzi wa kuchagua kati ya uadilifu na ufisadi,
udhaifu na uwajibikaji. Naomba wananchi wa Chalinze mchague CHADEMA,
mpigieni kura Mathayo Torongey. Mabadiliko ya Kweli, Uhuru wa Kweli.
Kwa maelezo zaidi wasiliana na Mratibu Mohamedi Mtoi kupitia 0784246764 au 0713246764.
Wenu katika demokrasia na maendeleo, John Mnyika (Mb) Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano Bungeni, Dodoma
No comments:
Post a Comment