Pages

Saturday, April 5, 2014

JOHN MNYIKA ATOA UJUMBE KWA WANANCHI WA CHALINZE

Leo Jumamosi 05 Aprili 2014 ni siku ya mwisho ya kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chalinze na kesho Jumapili 06 Aprili 2014 ni siku ya wananchi kupiga kura.

Kwa wananchi wa Jimbo la Chalinze wa kata mbalimbali mnaoweza kupata ujumbe kwa njia ya mtandao nawajulisha kwamba nitazungumza nanyi katika mkutano wa hadhara leo.

Kampeni za Chalinze zilizinduliwa na Katibu Mkuu Dr. Wilbroad Slaa na zitafungwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Said Issa Mohamed (ZNZ) akiwa na Dr. Slaa.

Kwa wapenda demokrasia na maendeleo popote mlipo ziungeni mkono timu za viongozi, wanachama na wapenzi kwenye kata na vijiji mbalimbali.

Wasiokuwa na mtandao naamini timu zetu za kampeni ya chini kwa chini na zenye magari ya matangazo kwa pamoja zitakuwa zimeshawaalika kwa kuzingatia ratiba ya kampeni. Tutahutubia kufunga kampeni kupitia mkutano utakaofanyika eneo la Chalinze Mjini (Sokoni) kuanzia saa 8 mchana mpaka 12 jioni, nitakuwepo pamoja na viongozi wengine wa kitaifa.

Naandika ujumbe huu kwa wananchi wa Chalinze walio nje ya jimbo hilo katika wilaya za jirani kufanya kila linalowezekana kurejea kwenda kupiga kura ama walau muwasiliane na ndugu, jamaa na marafiki walio katika kata na vijiji mbalimbali kujitokeza kupiga kura kesho na kuchagua mabadiliko.

Huu ni zaidi ya uchaguzi, ni uchaguzi kati ya wanyonge na wenye mamlaka, ni uchaguzi kati ya wakataa usultani na wakumbatia usultani, ni uchaguzi kati ya walioshindwa kuboresha huduma na kuanza kutoa ahadi nyingine za kilaghai dhidi ya wanaozijua shida na kero na walio tayari kuzitatua. Ni uchaguzi wa kukataa ghiliba.

Kesho ni kwenda kupiga kura kwa CHADEMA kwa lengo la muda mfupi la kuongeza mbunge mwingine wa upinzani na kupunguza hodhi ya chama kimoja bungeni kuongeza nguvu yetu ya kuwakilisha wananchi na kuisimamia Serikali.

Kesho ni kwenda kupiga kura za ushindi kwa CHADEMA kuipunguzia kura CCM kwa lengo la muda wa kati la kuiondoa CCM madarakani katika chaguzi zijazo kwa kuikataa kuanzia sasa ili kuleta uongozi bora, sera sahihi na mikakati makini kwa maendeleo endelevu ya nchi yetu na wananchi wake.

Sababu zipo nyingi; nieleze chache na zingine nitazieleza mkutanoni. CCM imekuwa ikitoa ahadi lukuki lakini utekelezaji ni kiduchu:

Mosi, Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005 kupitia ahadi za papo kwa papo na Ilani ya Uchaguzi ya CCM alitoa ahadi nyingi kwa Chalinze na nchi nzima kwa ujumla. Kati ya ahadi hizo ni pamoja na ile ya ‘maisha bora kwa kila mtanzania’ ambayo utekelezaji wake umefanyika kinyume chake kwa kuwaongezea mzigo mkubwa wa gharama na ugumu wa maisha kwa wananchi.

Kazi ya mbunge ni kuisimamia serikali kuwezesha maendeleo. Hivyo Chalinze chagueni Mbunge kupitia CHADEMA Mathayo Torongey kwa kuwa atakuwa huru ‘kuibana’ Serikali inayoongozwa na Rais Kikwete kuliko mbunge wa CCM.

Pili, “Mabadiliko ya Kweli hayawezi kuletwa na mafisadi wale wale wa chama kile kile kile chenye uoza ule ule, wakiendeleza yale yale; eti kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya. Kwa falsafa ya chukua chako mapema, Tanzania yenye neema haiwezekani”, hii ni nukuu kutoka Ilani ya Uchaguzi ya CHADEMA ya mwaka 2005 kwenye sera yake ya ‘mfumo mpya wa utawala’.

Wakati wa uchaguzi huo mapambano dhidi ya mafisadi hayakuibua mjadala mkubwa wa kitaifa, hata hivyo madai mengi ya wakati huo yakadhihirika tarehe 15 Septemba 2007 kupitia orodha ya mafisadi. Ikumbukwe kwamba tarehe 16 Disemba 1959, Mwalimu Nyerere alitangaza maadui watatu wa taifa ambao ni umaskini, ujinga na maradhi.

Tarehe 17 Mei 1960 alitoa kauli bungeni ya kuongeza adui mwingine mkubwa zaidi na namnukuu: “Napenda kuongeza adui mwingine katika orodha ya maadui wanaoitesa jamii yetu, ambao ni umaskini, ujinga na maradhi. Kwa hakika, tunaweza kufanya juhudi za kushughulikia tatizo la umaskini.

“Tunaweza kufanya juhudi za kushughulikia tatizo la ujinga, pia tunaweza kufanya juhudi za kushughulikia tatizo la maradhi. Lakini juhudi hizo hazitazaa matunda endapo wananchi hawatakuwa na imani na Serikali yao. Endapo hawatakuwa na imani na uadilifu wa viongozi watakaopewa madaraka na Serikali, kutokana na viongozi hao kuwa ni wala rushwa.

"Lazima niwe mkweli. Nasema kwamba rushwa ipo. Kwa hiyo, Mhe. Spika, lazima rushwa ipigwe vita sana kwa sababu naamini kuwa; rushwa ni adui anayeleta madhara makubwa zaidi kwa wananchi wakati wa amani, kuliko madhara yanayosababishwa na vita wakati wa vita. Mimi naona kuwa, kosa la rushwa linastahili kuwekwa katika kiwango kilicho sawa na kosa la uhaini, kwa sababu linaondoa kabisa imani ya wananchi kwa Serikali yako”.

Kwa wosia huo wa Mwalimu Nyerere kuichagua CCM ambayo imehusishwa na ufisadi wa Fedha za Malipo ya Akaunti ya Nje (EPA) kupitia kampuni ya Kagoda na ufisadi mwingine mwingi kwa nyakati mbalimbali ni kumkumbatia adui mwenye madhara kuliko vita.

Adhabu ya uhaini huwa ni kifungo kirefu au hata kifo, kwa maneno ya Mwalimu Nyerere mafisadi wanastahili adhabu sawa na wahaini; kifo au kifungo cha mafisadi wa kisiasa ni kuwakataa katika sanduku la kura.

Hivyo, hata bila kujali CHADEMA imemsimamisha mgombea gani; wananchi wa Chalinze wanapaswa kuacha kuipa kura CCM na kuchagua CHADEMA ambayo imeonyesha dira na dhamira katika dhima yake ya kupambana na ufisadi.

Uadilifu wa Mathayo Torongey ni mkubwa kuliko wa Ridhwani Kikwete, hivyo ili kusimamia vizuri rasilimali za umma katika Halmashauri na Bungeni kuchangia katika maendeleo ya Chalinze na Taifa. Hivyo, leo tuungane kutafuta kura za CHADEMA kesho zipigwe na tuzilinde kuwezesha mabadiliko.

Tatu, CHADEMA ni chama chenye sera mbadala kinachopaswa kupigiwa kura na wananchi kiongeze nguvu za kuzisimamia.

Sikuwa na mpango wa kuja Chalinze kwenye kampeni kwa kuamini kwamba viongozi wenzangu walio nje ya Bunge Maalum wanatosha kumaliza kampeni. Hata hivyo, yanayojiri katika Bunge Maalum yamenifanya niamue kutumia fursa hii ya kampeni kufikisha ujumbe kwa wananchi na kuhamasisha mabadiliko.

Itakumbukwa kuwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 CHADEMA kiliahidi kuanzisha mchakato wa katiba mpya ndani ya Siku 90/100 za utawala.

Pamoja na kuwa hakikutangazwa kuingia madarakani kiliamua kusimamia sera hiyo kwa wabunge kususia hotuba ya Rais Kikwete bungeni, kutangaza kutoyatambua matokeo ya urais na kushinikiza mchakato wa kuandika katiba mpya uanze. Ndani ya siku 100 Rais Kikwete akatangaza kuanzisha mchakato.

Hata hivyo, kwa kuwa hakukuwa na dhamira njema ndani ya Serikali na CCM toka kuanza kwa mchakato huo kumekuwa kukitungwa sheria mbovu mbovu zenye kuchelewesha na ‘kuchakachua’ mchakato katika hatua mbalimbali.

Katika hatua ya sasa Rais ametumia vibaya madaraka makubwa aliyokuwa amepewa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kuteua viongozi, makada na mawakala wengi wa CCM miongoni mwa wajumbe 201 wa Bunge Maalum.

Hatimaye akalihutubia Bunge Maalum na kwenda kinyume kabisa na misingi muhimu ya rasimu ya katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Izingatiwe kwamba Rais angeweza kutoa maoni yake rasimu ya kwanza ilipotolewa, hakufanya hivyo na kuamua kwenda kupinga rasimu ambayo imewasilishwa Bungeni kwa maelekezo yake. Rais amesababisha kwamba katika Kamati za Bunge Maalum wajumbe wengi wanaotokana na chama chake au aliowateua wanamtumia yeye kama rejea badala ya ripoti za maoni ya wananchi na utafiti wa wataalamu.

Pamoja na ‘kuchakachua’ rasimu ya katiba kuondoa muundo wa Muungano wa Shirikisho la Serikali tatu na kuingiza muundo ule ule wa Serikali mbili kama ilivyo katika Katiba ya mwaka 1977. Wajumbe hao wamefikia hatua hata ya kupiga kura ya ibara za rasimu wakitaka hata masuala mengine kwenye tunu za taifa mathalani uzalendo, uwazi na uwajibikaji yaondolewe.

Kura za wajumbe kufikisha theluthi mbili (2/3) kuwezesha ‘uchakachuaji’ huo hazikutokana na uteuzi tu bali pia zinatafutwa kwa njia nyingie za vitisho na za kifisadi. Katika hali ya sasa sioni dalili za mchakato huu kusonga mbele, utakwamia katika mjadala wa sura ya kwanza na sura ya sita.

Mjadala huu utaibuka katika Bunge la Bajeti ambapo mbunge mpya wa Chalinze atakuwa amepatikana. Naomba wananchi mumchague Mathayo Torongey CHADEMA tupate mbunge mwingine ili ukija mjadala wa muswada mwingine wa sheria unaohusiana na sheria ya mabadiliko ya katiba au kura ya maoni kuwe na sauti nyingine ya kuisimamia Serikali.

Tusitarajie kwamba Ridhwani ataweza kupinga miswada mibovu inayoletwa bungeni baada ya kupitishwa na baraza la mawaziri chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete. Huu ni uchaguzi wa kuchagua kati ya uadilifu na ufisadi, udhaifu na uwajibikaji. Naomba wananchi wa Chalinze mchague CHADEMA, mpigieni kura Mathayo Torongey. Mabadiliko ya Kweli, Uhuru wa Kweli.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na Mratibu Mohamedi Mtoi kupitia 0784246764 au 0713246764.
Wenu katika demokrasia na maendeleo, John Mnyika (Mb) Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano Bungeni, Dodoma

No comments:

Post a Comment