Thursday, July 17, 2014

DK.KIGWANGALA AUNGANA NA KAFULILA, ADAI KUNA WIZI MKUBWA UMEFANYIKA ESCROW



Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamis Kigwangala akiongea na wanahabari wa Global Publishers (hawapo pichani).

Makala: Elvan Stambuli
MBUNGE wa Nzega (CCM), Dk. Hamisi Kigwangala ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ameungana na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila kwa kudai kuwa ni kweli kuna wizi mkubwa umefanyika katika akaunti ya Escrow.
Akizungumza na safu hii Dk. Kigwangala alisema yeye siyo muumini wa ufisadi, hivyo kutokana na utafiti alioufanya ana hakika kuwa kuna wizi wa mabilioni ya shilingi katika akaunti hiyo ya  Escrow.
Katika mazungumzo hayo ambayo yalikuwa yakirekodiwa na ‘kruu’ ya Global TV Online mwishoni mwa wiki iliyopita ambayo yamerushwa leo hewani Dk. Kigwangala alifafanua:

Dk. Kigwangala: Escrow kuna ufisadi na sisi Chama Cha Mapinduzi tuna kiapo kwamba nitasema kweli daima na mimi ni mpinga ufisadi. Bungeni nilisema wazi kabisa kuwa katika hilo kuna ufisadi. Siwezi kutetea wizi ule. Kama tunataka kurudisha nidhamu (CCM) lazima walioiba wawajibishwe na siyo kutumia bunge kutetea wizi, kiongozi (anamtaja) anasema waziwazi uongo bungeni na wabunge wanamshangilia, nilishangaa sana.
Mwandishi: Nyinyi kama wabunge wizi huo unaodaiwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni 200 mtafanyaje kuhakikisha wanaodaiwa kuiba wanawajibishwa?

Dk. Kigwangala: Sasa hivi kuna uamuzi wa bunge na mapendekezo ya waziri mkuu yamefanyika. Kamati ya Bunge ya Mahesabu ya Zitto Kabwe wamepeleka suala hilo kwa CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali  nchini), achunguze na Takukuru wachunguze, wabunge wengine tumeambiwa tupeleke ushahidi kwa hili la Escrow kwenye vyombo hivyo. Mimi niko tayari kutoa maelezo yangu huko kwa sababu nimeona kuna harufu kubwa ya wizi na jambo hili bado halijafungwa. Huu mjadala bado upo na utakuja tena bungeni.
Mwandishi: Je, utagombea urais mwakani?
Dk. Kigwangala: Mpaka sasa sijatangaza nia ya kugombea urais au ubunge kwani bado natumikia wananchi. Lakini jimboni wanasema kwa nini nasitasita? Wazee, vijana, viongozi wa dini kule jimboni wanasema kwa nini nisiingie 2015 nami nimekuwa nawatia moyo kuwa tusubiri. Wanaonishashiwi ni wengi nami nawaambia wasubiri nitafakari kwa sababu kazi ya urais ni nzito kwani hii kazi ya ubunge yenyewe ni nzito. Natafakari kuangalia mchakato mzima. Hata kwenye ubunge natafakari.Tusiwe na haraka, muda ukifika nitasema.
Mwandishi: Mara baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka 2010 hadi sasa 2014 umefanya nini katika kuwaletea maendeleo wananchi wako?

Dk. Kingwangala: Watu wanaamini kuwa viongozi wa kuchaguliwa ndiyo wanaopaswa kutekeleza ahadi lakini sisi wabunge kazi yetu kubwa ni kutunga sheria na kuwakilisha wananchi, hivyo kazi ya utendaji haimo katika utendaji wa kazi za mbunge. Nzega napaswa kuisimamia serikali kutekeleza ahadi tulizoahidi kupitia kampeni za rais, sisi wabunge na madiwani. Ahadi hutekelezwa na serikali sasa ni lazima nihakikishe zinatekeleza.
Mwandishi: Je, ahadi hizo mlizozitoa kwa wapiga kura umesimamia zikatekelezwa?
Dk. Kigwangala: Ahadi moja kubwa ambayo haijatekelezwa ni maji kutoka Ziwa Victoria japokuwa tayari mchakato unaendelea.
Ahadi ya umeme vijijini tumepeleka, zaidi ya kilomita 85 zimefikiwa, tumesambaza katika shule na zahanati. Miradi mingine mikubwa niliyofanya mimi kama mbunge ni kutekeleza mradi wa kuhimiza kilimo cha biashara. Nimehamasisha kilimo cha pamba, tuna wakulima zaidi 50,000. Nimehamasisha kilimo cha alizeti, zahanati zaidi ya 20 tumejenga, shule za sekondari zaidi ya 20, shule za kidato cha tano na sita tumejenga nne, mbili zimekamilika na nimezifanya kwa ubunifu wangu.

Mwandishi: Vipi kuhusu uchimbwaji wa  madini, umewanufaisha wapiga kura wako?
Dk. Kigwangala: Nahakikisha tunapata faida katika uchimbaji wa dhahabu na faida tunazipeleka katika miradi mbalimbali ya wananchi, tumejenga barabara za lami, ipo ya kilimita 20 na tunajenga stendi mpya ya kisasa, soko na saccos zaidi ya kumi tumeanzisha.
Mwandishi: Je, uchaguzi ukija leo na ukagombea, unajihakikishia kuwa utashinda?
Dk. Kigwangala: Nitashinda kwa urahisi sana kwa sababu nimejikita katika kazi nilizofanya na wapigakura wanaona. Wananchi wanataka mtu atakayeweza kupambana na umaskini na maradhi na siyo makundi, mimi sina kundi jimboni.

Mwandishi: Unazungumziaje upatikanaji wa gesi Mtwara?
Dk. Kigwangala: Kwenye gesi kuna tatizo na sisi wenye uelewa lazima tueleze ukweli.
Kama taifa tumebarikiwa tumepata gesi. Watanzania wanadhani tumepata muarobaini wa matatizo baada ya kuipata. Lakini Tanzania tuna mbuga za wanyama, dhahabu, mafuta, tanzanite, ng’ombe nakadhalika na sasa tuna gesi lakini bado nchi ni maskini kwa sababu tumechanganyikiwa.
Lakini hatuna sera ya gesi na bungeni suala hilo lilikuwa halijajadiliwa.  Lazima tutunge sheria.
Hatuna haja ya kukurupuka kuuza vitalu mpaka tuwe na sera na sheria.
CHANZO GPL

No comments:

Post a Comment