Monday, April 7, 2014

TIMU YA TAIFA YA WATOTO MITAANI YANYAKUA KOMBE LA DUNIA


Timu ya taifa ya Tanzania ya watoto wa mitaani wakishikilia Kombe la Dunia walilonyakua Brazil
Timu ya taifa ya Tanzania kwa watoto wa mitaani imenyakua Kombe la Dunia kwa watoto wa mitaani, katika mashindano yaliyozishirikisha timu za mataifa mbalimbali duniani huko Rio de Janeiro, Brazil hapo jana.
Ikiwa imetinga fainali za Kombe la Dunia kwa watoto wa mitaani kwa mara ya pili mfululizo, timu hiyo ya Tanzania imeweza kutwaa Kombe la Dunia kwa Watoto wa Mitaani kama linavyojulikana Street Child World Cup hapa Rio de Janeiro.
Katika mechi ya fainali Tanzania iliibanjua Burundi iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kulinyakua kombe hili kwa Kuinyuka magoli 3-1 huku mchezaji kiungo mshambuliaji wa Tanzania Frank William akipiga magoli matatu na kuwa nyota wa mchezo. Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Tanzania ilikuwa ikiongoza kwa magoli 2-0. Kipindi cha pili iliongeza bao la tatu. Burundi iliweza kupata bao la kufutia machozi zikiwa zimebakia dakika nne mpira kumalizika.
Tanzania imetwaa ubingwa huo baada ya kuonyesha kiwango cha juu hata kuzishinda timu ngumu kama Burundi, Marekani, Indonesia, Nicarague, Ufilipino na Argentina.
Golikipa wa Tanzania Emmanuel ameweza kuchaguliwa kuwa golikipa bora wa michuano hii ya kombe la dunia.
Hii ilikuwa mara ya Pili kwa timu ya Tanzania kutinga fainali za michuano hiyo ya dunia kwa watoto wa mitaani inayofanyika siku chache kabla ya fainali za Kombe la Dunia kuanza mwezi Juni. Ikumbukwe kuwa fainali zilizopita za michuano hii kule Durban Afrika Kusini mwaka 2010 Tanzania ilifungwa na India katika fainali.
Mashindano haya hutambuliwa na Shirikisho la Soka Duniani, FIFA.

No comments:

Post a Comment