HUKU moto wa upotevu wa fedha za umma katika akaunti ya Tegeta Escrow ukiwa bado unawaka kufuatia mawaziri wawili, mwanasheria mkuu wa serikali, katibu mkuu mmoja na Bodi ya Tanesco kutakiwa kuwajibishwa, mali zinazomilikiwa na vigogo waliochotewa fedha hizo usipime.
Moja ya ghorofa la kifahari katika maghorofa yanayomilikiwa na vigogo wa Escrow.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa wanaotajwa kunufaika na fedha hizo, unaonyesha kuwa, pamoja na mambo mengine, wanamiliki majumba makubwa ya kifahari, yakiwemo maghorofa katika maeneo mbalimbali ya mikoa, ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Morogoro.
Mmoja wa wanaotajwa (jina linahifadhiwa kwa sasa) ana jumba kubwa la ghorofa mbili sehemu za Mbezi Beach, Dar, ambalo licha ya kuwa ya thamani kubwa, pia ukubwa wa eneo analomiliki, umemfanya pia kujenga bwawa kubwa la kuogelea.
“Aina ya maisha anayoishi huwezi kusema kama ni Mtanzania, kwa sababu haonyeshi kama anajua uwepo wa shida, kwa sababu watoto wake wote wanasoma nje ya nchi na zipo likizo ambazo hawarudi kwa vile wanasafiri nchi tofauti na wanazosoma kwa ajili ya matembezi tu.
“Acha hii nyumba, ana ghorofa pale Kariakoo lote limepangishwa na magari anayoendesha huyu bwana ni hatari. Nafikiri gari la thamani ndogo kabisa ni BMW analoendesha mkewe. Kuna watu wana fedha hadi wanaudhi aiseee,” alisema mkazi mmoja wa Mbezi Beach, anayedai kuishi jirani na mfanyabiashara huyo aliyenufaika na fedha za Escrow.
Kigogo mwingine mwenye asili ya Mwanza, anadaiwa kununua jengo lenye ghorofa nne lililopo katikati ya Jiji la Mwanza na limeshaanza kufanyiwa marekebisho, kwani ana lengo la kuifanya hoteli.
Wakati ikiwa bado haijafahamika kama watu hao walionufaika na fedha hizo mali zao watafilisiwa au la, habari zinasema baadhi ya waliochotewa, wamekuwa na maisha ya kufuru, kutokana na matumizi ya kutisha ya fedha wanayofanya, huku wakinunua vitu mbalimbali vya thamani.
Hata hivyo, wakati watu hao wachache wakiwa wamegawana kiasi cha shilingi bilioni 306, idadi kubwa ya Watanzania wanaishi maisha ya umaskini mkubwa, kiasi cha kula mlo mmoja kwa siku, huku wakikosa huduma muhimu kama maji safi na salama ya kunywa, huduma bora za afya na elimu.
Mamia ya vituo vya afya vinavyomilikiwa na serikali huko vijijini havina dawa, hasa kipindi hiki ambacho serikali inadaiwa kiasi cha shilingi bilioni 90 na Bohari Kuu ya Madawa (MSD). Kutokana na kukosekana kwa dawa, Watanzania wengi hufariki dunia kwani zahanati nyingi zina dawa ndogondogo kama panado za kutuliza maumivu tu.
Muonekano wa ndani wa ghorofa hiyo.
“Wakati wengine wanakufa kwa kukosa dawa, shule zikiwa hazina vifaa vya kufundishia na uhakika wa kula ukiwa mdogo, Watanzania wengine wanaishi kifalme, wanapata kila kitu wanachotaka, wanakwenda popote wanapotaka, wanatibiwa hospitali wanazotaka. Bora maisha wanayoishi yangekuwa kwa sababu ya fedha halali, lakini hizi za wizi ni hatari sana,” alisema mwanaharakati mmoja, aliyejitaja kwa jina moja la Nando.
Wiki iliyopita, Bunge lilitoa maazimio nane yanayotakiwa kutekelezwa na serikali, ikiwa ni pamoja na kupendekeza mamlaka ya uteuzi kuwavua nyadhifa zao Mawaziri Sospeter Muhongo na Anna Tibaijuka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakim Maswi pamoja na kuvunjwa kwa Bodi ya Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco).
Bunge hilo pia, lilimjadili Singasinga Harbinder Sigh Seth (pichani) ambaye inadaiwa ndiye kinara wa dili hilo.
No comments:
Post a Comment