Watu kumi wamekufa, na mamia kukosa mahali pa kuishi kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Kamishna Suleiman Kova, amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo,
ambapo alisema kati ya watu hao kumi, watano ni watu wazima na watoto
watano.
Mvua kubwa zilizonyesha mfululizo
kuanzia Ijumaa maeneo mbalimbali jini Dar es Salaam zimesababisha vifo
hivyo na kuharibu miundombinu ya barabara yakiwemo madaraja sita
kubomolewa na maji ya mvua hizo.
Waandishi wa BBC jijini Dar es Salaam
waliozunguka maeneo mbalimbali ya jiji hilo wameshuhudia uharibifu
mkubwa wa miundombinu, mali na makaazi ya watu.
Daraja la Mpiji linalounganisha wilaya ya
Kinondoni katika mkoa wa Dar es Salaam na Bagamoyo mkoa wa Pwani
limekatika na kupoteza mawasiliano kati ya mikoa hiyo miwili.
Waziri wa Ujenzi, Dr. John Magufuli alifika
Jumamosi katika eneo la tukio na kusema serikali italifunga daraja hilo
kwa siku mbili wakati kazi ya ukarabati ikifanyika ili kuharakisha
urejeshaji wa mawasiliano kati ya mikoa hiyo.
Watu walioathirika zaidi kutokana na mafuriko
hayo ni watu waliojenga mabondeni, hasa maeneo ya Jangwani, na bonde
lote la mto Msimbazi.
Wakaazi hawa ambao mara kwa mara hukumbwa na
kadhia hii hata pale mvua ndogo zinaponyesha, hali ya sasa imekuwa
tishio zaidi kwa maisha yao na mali, huku mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,
Sadiq Meck Sadiq akisema serikali haitaweza kuendelea kuwasaidia
waathirika hawa, ambao wanapuuza wito unaotolewa mara kwa mara kuwataka
kuyahama maeneo hayo hatarishi, na wengine hata kwenda mahakamani
kupinga amri ya kuwataka kuhama.
Mwaka 2012, serikali ya mkoa wa Dar es Salaam
iliwataka wakaazi wa bonde la Jangwani waliokuwa wameathiriwa na
mafuriko kuhamia katika maeneo salama likiwemo eneo la Mabwepande nje
kidogo ya jiji la Dar es Salaam ambako waligawiwa viwanja.
Hata hivyo baadhi yao waligoma kuhama na wale
waliohama wanadaiwa wengine walivitelekeza viwanja walivyogawiwa na
kurejea katika maeneo yao ya mabondeni.
Mradi mwingine muhimu wa Mabasi yaendayo kasi,
DART unaolenga kutatua tatizo la usafiri jijini Dar es Salaam, nao
umeathiriwa na mvua zinazonyesha na kusababisha hasara ya kiasi cha dola
elfu thelathini za Kimarekani kutokana na magari yake matatu kuharibiwa
pamoja na mashine nyingine na mifuko ya saruji kuchukuliwa na maji
hivyo kusitisha shughuli zake za ujenzi zilizo katika hatua za mwisho
kukamilika kwa barabara ya Mbezi hadi Kivukoni katikati ya jiji.
No comments:
Post a Comment